Alexandria, Misri
Mambo si mambo kwa klabu ya Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Al Ahly ya Misti, mechi iliyopigwa usiku wa Ijumaa, Januari 24, 2026 kwenye Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
Yanga ambayo ipo Kundi B ilitunguliwa mabao hayo na Mahmoud Hassan Trezeguet, mabao yaliyowafanya wababe hao wa Misri na Afrika kuongoza kundi hilo ambalo pia lina timu za JS Kablie ya Algeria na AS FAR Rabat ya Morocco.
Ahly licha ya kuwa wenyeji na kutawala mchezo lakini mechi haikuwa rahisi kwao kwani kwa kipindi chote cha kwanza walipata wakati mgumu kuupenya ukuta wa Yanga kabla ya kuwaotea katika dakika za nyongeza za kipindi hicho kwa bao la Trezeguet.
Mpira uliozaa bao hilo ulitokana na krosi ya Mohamed Hany kutokea na kumkuta Trezeguet aliyeruka juu na kuujaza mpira wavuni kwa kichwa akimuacha kipa wa Yanga, Djigui Diara akiwa hajui la kufanya.
Umakini na mbinu za uwezo wa Ahly kutawala mchezo ulizaa matunda katika dakika ya 75 walipopata bao la pili, safari hii Trezeguet aliunasa mpira akiwa katika eneo la penalti na kuuhamishia kwenye mguu wake wa kulia kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni.
Baada ya matokeo hayo, Al Ahly sasa imefikisha pointi saba ikiwa kinara wa kundi hilo wakati Yanga inabaki katika nafasi ya pili na pointi zake nne ikiwa imeshinda mechi moja na sare moja.
Kimataifa Yanga yakwama Misri, yalala 2-0
Yanga yakwama Misri, yalala 2-0
Read also
