London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema anaaamini hakuna mtu mwenye shauku na njaa ya kutaka Arsenal ibebe taji la Ligi Kuu England (EPL) kumzidi yeye.
Arsenal imekuwa ikipambana kwa udi na uvumba kusaka taji la EPL kwa miaka kadhaa sasa lakini nguvu hizo zimekuwa zikikwama wakati mwingine katika hatua za mwisho na mara ya mwisho ililibeba taji hilo mwaka 2004.
Katika mbio za kulisaka taji hilo kwa miaka ya karibuni, Arsenal ilichofanikiwa ni kushika nafasi ya pili katika misimu mitatu.
Msimu huu unaoendelea wa 2025-26, matumaini yameendelea kuwa makubwa Arsenal ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi saba lakini bado zimebaki mechi 16 kabla ya ligi kufikia tamati hivyo kazi bado ipo.
Matumaini ya Arsenal kwa kiasi kikubwa yanabebwa na mwenendo usiovutia wa Man City ingawa kwa mechi 16 zilizobaki kabla ya ligi kumalizika lolote linaweza kutokea.
Akizungumzia mbio za kulisaka taji hilo wakati timu yake kesho Jumapili Januari 25, 2026 ikiumana na Man United nyumbani kwenye dimba la Emirates, Arteta alisema anadhani hakuna mtu mwenye tamaa na shauku ya kulibeba taji hilo kumzidi yeye.
“Lakini tunajua kwamba namna pekee ya kufanikisha hilo ni kuwa makini, kuwa vizuri kwa kila tukio na kwa kila kile tunachokifanya leo kukifanya vizuri zaidi kesho,” alisema Arteta.
Arteta alifafanua kwamba hiyo ndiyo hali halisi na ndilo jambo lililo katika uwezo wao mengineyo hayaongezi chochote kwao na yanaweza kuwatoa na kuwafanya wawe makini na mambo tofauti.
