Na mwandishi wetu
Kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama amerejea katika klabu yake ya Simba na tayari ameungana na wachezaji wenzake wa timu hiyo walioelekea Tunisia kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Chama amejiunga na Simba akitokea Singida Black Stars hatua ambayo inamfanya kurudi kwa mara nyingine katika klabu hiyo aliyoichezea kwa mafanikio makubwa kabla ya kuihama.
Chama alijiunga na Simba mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia na baada ya kutamba akiwa mmoja wa wachezaji tegemeo alisajiliwa na RS Berkane ya Morocco Agosti 2021 lakini mambo hayakwenda vizuri na Januari 2022 alirudi tena Simba.
Uwezo na umahiri wa CHama vilijidhihirisha kwa namna alivyotoa mchango mkubwa kwa Simba kwenye ligi ya Tanzania na Afrika kabla ya kuachana na Simba Julai 2024 na kujiunga na mahasimu wao Yanga.
Alidumu Yanga kwa msimu mmoja kabla ya kutimkia Singida Black Stars Septemba mwaka jana lakini Januari mwaka huu amekuwa habari kubwa baada ya kurudi Simba akitajwa kama mchezaji aliyerudi nyumbani.
Jumamosi hii Januari 24, 2026, Simba itaumana na Esperance ya Tunisa, katika Ligi ya Mabingwa ambapo Chama anatajwa kuziba pengo la Jean Ahoua, kiungo wa Simba aliyeihama timu hiyo hivi karibuni na kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria.
Simba ambayo ipo Kundi D katika Ligi ya Mabingwa, mwenendo wake si mzuri katika michuano hiyo kwa msimu huu na kumekuwapo hali ya wasiwasi kwamba huenda timu hiyo ikaishia hatua ya makundi.
Soka Chama arudi Simba, aelekea Tunisia
Chama arudi Simba, aelekea Tunisia
Read also
