Mdrid, Hispania
Winga wa Real Madrid, Vinícius Júnior ametumia mitandao ya kijamii kumdhihaki kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone kwa kumwambia kuwa amepoteza pambano jingine la mtoano.
Kauli hiyo ya Vinicius, ‘Vinicius Jr’ au ‘Vini’ imeambatana na picha ya video ikihusisha mechi baina ya timu hiyo iliyochezwa Alhamisi Januari 8, 2026 na Real Madrid kushinda kwa mabao 2-1.
Katika mechi hiyo ya nusu fainali ya Spanish Supercopa iliyopigwa mjini Jeddah, Saudi Arabia, mjadala wa baada ya mechi ulihusisha utata uliojitokeza baina ya Vini na Simeone wakati wa mechi.
Kamera za televisheni ziliwaonesha wawili hao wakizozana katika kipindi cha kwanza kuhusu madai ya Atletico kutaka wapewe penalti huku Simeone akimwambia Vini zaidi ya mara moja kwamba ataachwa na Real Madrid.
Baadaye, Simeone na Vini wote walipewa kadi za njano kutokana na mzozo huo wa maneno kabla ya kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso na wasaidizi wake kuingilia kati na baadaye Vini kufanyiwa mabadiliko.
Simeone alipotakiwa kutoa maoni yake baada ya mechi alisema hakumbuki nini alikisema kwa kuwa ya uwanjani yanabaki uwanjani.
“Sina la kusema, mambo yanayotokea uwanjani yanabaki uwanjani, sina kumbukumbu, mimi si mtu mwenye kumbukumbu nzuri,” slisema Simeone.
Kwa upande wake Alonso alisema hakufurahishwa na tabia za Simeone na hakulipenda tukio zima baina ya Vini na Simeone hasa kauli za Simeone.
“Sijapenda kilichotokea, hayo mambo yamevuka mipaka katika suala zima la kuheshimu mwenzako, alichokisema (Simeone) si mfano wa tabia za mwanamichezo mstaarabu, kuna mipaka,” alisema Alonso.
Baadaye ndipo Vini alipotumia mtandao wa Instgram kutoa maoni yalioonekana kumdhihaki Simeone akidai kocha huyo amepoteza pambano jingine la mtoano, maoni yaliyoambatana na picha ya tukio la mzozo wake na Simeone.
Real Madrid ambao sasa watacheza mechi ya fainali na mahasimu wao Barca, ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Federico Valverde kwa mpira wa adhabu na baadaye Rodrygo akaongeza la pili wakati bao pekee la Atletico lilifungwa na Alexander Sorloth.
