Rabat, Morocco
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah amepuuza habari inayoiweka timu yao katika orodha ya timu zinazopewa nafasi kubwa kubeba taji ya michuano ya Afcon 2025 inayoendelea nchini Morocco.
Salah ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Liverpool ya England, badala yake amesema kwamba wanachofanya katika fainali za Afcon ni kuweka mkazo kwa kila mechi wanayocheza.
Misri kwa sasa inapambana kusaka taji la nane la Afcon, tayari imefuzu hatua ya robo fainali baada ya kuichapa Benin mabao 3-1 huku Salah akiwa moto kwenye mechi hiyo akifunga bao la tatu na hadi sasa ana mabao matatu katika fainali hizo.
Timu hiyo imeonesha kiwango cha kuvutia katika Afcon 2025 lakini Salah yuko makini katika matarajio makubwa ambayo yanahusishwa na timu hiyo kwa kupewa nafasi kubwa ya kubeba taji.
“Tuna wachezaji wachanga na wengi wao wanacheza soka nyumbani Misri, tunachofanya ni kuipigania nchi yetu na baada ya hapo tutaona tutakapofika, kila mmoja hapa anataka kujitoa katika ubora wake,” alisema Salah.
Katika fainali za Afcon zinazoendelea, Salah hadi sasa amekosa mechi moja ya hatua ya makundi dhidi ya Angola, mechi ambayo Misri walicheza wakiwa tayari wamefuzu hatua ya mtoano (16 bora) na kukutana na Benin.
Uamuzi wa kocha Hossam Hassan kumuweka benchi mchezaji huyo ulionekana kuwa na faida kubwa kwa namna ambavyo alikuwa tishio katika mechi dhidi ya timu sumbufu ya Benin na hatimaye kutoka na ushindi.
Salah pia aliipongeza Benin akisema kwamba Misri ilicheza dhidi ya timu nzuri yenye kocha bora na mfumo mzuri na wana furaha kwa kupata ushindi ingawa anakiri haikuwa kazi rahisi.
.
