Manchester, England
Klabu ya Manchester United imemfuta kazi kocha Ruben Amorim baada ya kushikilia wadhifa huo kwa kipindi kisichozidi miezi 14.
Uamuzi huo umetangazwa leo Jumatatu, Januari 5, 2026 ikiwa ni siku moja baada ya timu hiyo kutoka sare ya bao 1-1 na Leeds United na kocha huyo kunukuliwa akitoa hoja ya kuwataka mabosi wa klabu wafanye kazi yao.
Baada ya kutimuliwa kwa Amorim, nafasi yake itashikwa kwa muda na Darren Fletcher ambaye ni kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 18 ya klabu hiyo na ataiongoza katika mechi ya keshokutwa Jumatano dhidi ya Burnley.
Habari za ndani zinadai kwamba mabosi wa Man United kwa sasa wapo katika mchakato wa kumpata kocha wa kuongoza timu hiyo kwa kipindi cha mpito hadi mwisho wa msimu huku taratibu za kumpata kocha wa kudumu zikiendelea.
Baada ya kufikia uamuzi wa kumtimua Amorim, kocha huyo aliarifiwa jambo hilo mapema leo Jumatatu katika mazungumzo ya ana kwa ana na mkurugenzi wa soka, Jason Wilcox pamoja na ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Omar Berrada.
Kwa siku za karibuni zimekuwapo habari kwamba Amorim hana maelewano mazuri na Wilcox na inadaiwa ndiyo sababu mojawapo ya kutimuliwa kwa kocha huyo hasa baada ya mazungumzo mazito katika kikao cha wawili hao kilichofanyika Ijumaa iliyopita.
Habari zaidi zinadai kwamba tatizo mojawapo la Amorim ni msimamo wake wa kuutumia mfumo wa 3-4-3 na katika kikao na Wilcox, mada kuhusu mfumo huo ilimkera kocha huyo ikiwamo mada iliyohusu sare ya bao 1-1 dhidi ya Wolves siku tatu zilizopita.
Klabu hiyo hata hivyo imeipinga hoja hiyo badala yake imedai kuwa sababu hasa ya kutimuliwa kwa Amorim ni kocha huyo kutoonesha dalili za kutosha za kuleta mabadiliko kwenye timu.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Amorim hakuwa katika hali ya kawaida na baadaye hakuwa tayari kwa mahojiano kwa alichodai kuwa ni sababu binafsi na kumuachia jukumu hilo beki Lisandro Martinez.
Amorim anaachana na Man United akiwa na rekodi ya kushinda mechi 25, sare 15 na kupoteza mechi 23 tangu akabidhiwe tumu hiyo kutoka kwa Erik ten Hag.
Ten Hag alitimuliwa Oktoba 28, 2024 na nafasi yake ilishikwa kwa mwezi mmoja na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Ruud van Nistelrooy na baada ya hapo Amorim akabeba majukumu hadi kutimuliwa kwake hii leo.
Kimataifa Amorim afutwa kazi Man United
Amorim afutwa kazi Man United
Read also
