Rabat, Morocco
Umewahi kusikia hadithi ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufa kiume, achana na hadithi zote za nyuma, hadithi ya kweli imetokea leo Jumapili Januari 4, 2026 kwa timu hiyo kufungwa bao 1-0 na Morocco kwenye fainali za Afcon 2025.
Stars ikiumana na wenyeji Morocco katika mechi ya hatua ya mtoano (16 bora) imekubali kipigo hicho na hivyo kuaga fainali hizo huku ikiweka rekodi ya kipekee kwa kupambana kisawasawa na Morocco ambao ni wenyeji wa fainali hizo.
Matarajio ya Stars kufungwa mabao mengi yalitoweka na hadi dakika 90 zinamalizika Morocco, timu lenye hadhi na heshima yake katika soka, Afrika na duniani kote, ilishikwa kila kona na kujikuta ikiambulia bao hilo pekee.
Morocco ambao kwa ushindi huo wamefuzu hatua ya robo fainali, waliuanza mchezo kwa kufanya mashambulizi na kuongoza kwa umiliki wa mpira kwa zaidi ya asilimia 70 katika kipindi chote cha kwanza lakini nidhamu ya safu ya ulinzi ya Stars ilikuwa kikwazo.
Safu hiyo ya ulinzi ya Stars ilifanikiwa kuwavuruga Morocco mbele ya maelfu ya mashabiki wao ambao licha ya kushangilia kwa muda mwingi, hawakuamini kuona timu zikitoka uwanjani kwenda mapumziko bila kufungana.
Moja ya nafasi ambazo Morocco walizitengeneza lakini hazikuweza kuwapatia bao ni katika dakika ya 24 baada ya Ismail Saibari kuuwahi mpira wa juu na kuujaza wavuni kwa kichwa lakini mwamuzi alikataa bao hilo baada ya kutumia VAR kwa madai kwamba mfungaji aliotea.
Stars ambao wanajivunia rekodi ya kufikia hatua ya mtoano ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza, nao walifanya mashambulizi kadhaa kwa nidhamu ya hali ya juu, mfano katika kipindi hicho Simon Msuva akiwa ndani ya 18 alishindwa kuunganisha vyema krosi ya Seleman Abdallah.
Kipindi cha pili juhudi za Morocco zilizaa matunda dakika ya 63 baada ya kupata bao hilo pekee lililotokana na shuti la chini lililopigwa na mshambuliaji wa Real Madrid, Brahim Diaz na kujaa wavuni huku kipa Hussein Masalanga akiishia kuugusa mpira huo na mkono wake wa kushoto.
Stars, licha ya kufungwa bao hilo lakini waliendelea kuonesha upambanaji bila kujali aina ya mpinzani waliyekuwa wakishindana naye na katika dakika za lala salama, Iddi Nado aliangushwa na beki wa Morocco, Adam Masina wakati akiambaa na mpira kuelekea lango la Morocco.
Kuangushwa kwa mchezaji huyu kuliibua malalamiko kwa wachezaji na benchi la Stars wakitaka wapewe penalti au VAR itumike ili kujua undani wa tukio hilo lakini mwamuzi wa mechi hiyo, Boubou Traore alikataa kutoa penalti.
Wakati Stars ikiziaga fainali hizo ikiwa kifua mbele, Morocco sasa wanasubiri kuumana na mshindi wa mechi kati ya Afrika Kusini na Cameroon katika mechi ya robo fainali.
Kimataifa Taifa Stars yafa kiume
Taifa Stars yafa kiume
Read also
