Libreville, Gabon
Serikali nchini Gabon imechukua uamuzi mgumu wa kuifuta timu ya taifa baada ya kufanya vibaya kwenye fainali za Afcon zinazoendelea nchini Morocco.
Sambamba na hilo, serikali hiyo pia imemuondoa katika kikosi hicho mshambuliaji mkongwe wa timu hiyo, Pierre-Emerick Aubameyang pamoja na kumfuta kazi kocha mkuu wa timu hiyo, Thierry Mouyouma na kulivunja benchi zima la ufundi.
Vipigo mfulululizo vimeifanya timu hiyo iage mapema fainali za Afcon ikianza kwa kuchapwa bao 1-0 na mahasmu wao Cameroon kabla ya kukutana na kichapo cha mabao 3-2 mbele ya Msumbiji.
Uamuzi huo wa Serikali ya Gabon umechukuliwa ikiaminika sababu ikiaminika kuwa ni kutofurahishwa na mwenendo mzima wa timu hiyo kwenye Afcon na inadaiwa hatua nyingine zitafuata baada ya uamuzi huo.
“Kwa kuzingatia madhara ya jumla ya mwenendo wa timu, serikali imeamua kulivunja benchi zima la ufundi kuifuta timu ya taifa hadi uamuzi mwingine utakapofikiwa na kuwaondoa katika timu hiyo wachezaji Bruno Ecuélé Manga na Pierre-Emerick Aubameyang,”ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Waziri wa Michezo wa Gabon, Simplice-Desire Mamboula.
Aubameyang (pichani juu) na Ecuele Manga ambao awali walijiuzulu kuichezea timu hiyo kabla ya kubadili maamuzi na kuitwa katika kikosi hicho, kila mmoja wao alikuwa nahodha katika mechi mbili za awali za Afcon.
Kitendo cha Aubameyang ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 36, kurudi katika timu hiyo kiliwashangaza baadhi ya watu kwa kuwa alikuwa akijiuguza baada ya kuumia wakati akiitumikia timu ya Marseille ya Ufaransa kabla ya kuanza kwa fainali za Afcon.
Kwa upande wake, Aubameyang alijitetea akisema kwamba anadhani matatizo ya timu ya taifa ya Gabon ni makubwa kuliko kumuangalia yeye mtu mmoja.
Uamuzi huo wa serikali hata hivyo huenda ukaiingiza nchi hiyo katika mgogoro na Fifa kwa kuwa kanuni za Fifa haziruhusu serikali kujiingiza na kuchukua hatua katika masuala yahusuyo soka.
