Rabat, Morocco
Kocha wa timu ya taifa ya Nigeria, Eric Chelle amewajia juu wachambuzi waliokuwa wakimkosoa baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tunisia kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.
Matokeo hayo ya mechi ya hatua ya makundi yaliibua shutuma dhidi ya Chelle kutokana na mabadiliko ya wachezaji aliyokuwa akiyafanya kocha huyo ambapo mashabiki na wachambuzi hawakuyakubali.
Kelele za mashabiki na hoja za wachambuzi zilitokana na mtazamo hasi kuhusu mabadiliko ambayo yalionekana kuibua hofu kwamba Nigeria ingeweza kupoteza ponti tatu katika mechi ambayo walionekana kuitawala vyema.
Chelle (pichani juu) hata hivyo alieleza kushangazwa kwake na mtazamo huo hasa kwa kuwa hakuna ambaye anazungumzia hali ilivyokwa katika mechi hiyo kwa kipindi cha kwanza hadi dakika ya 75 na jinsi kasi ya mchezo ilivyokuwa.
Kocha huyo alisema kwamba watu hawazungumzii kuhusu mbinu na hadhi ya wachezaji au namna ambavyo timu ilikuwa na haki ya kushinda na imepata ushindi mkubwa.
“Katika mechi hii tulikuwa vizuri kwa dakika 75, hadi mwishoni mwa kipindi cha kwanza tulitawala mchezo kwa asilimia 70 na hadi inafika dakika ya 75 tulikuwa timu bora uwanjani kwa hiyo nina furaha na najivunia wachezaji wangu,” alisema Chelle.
Malalamiko mengi yalikwenda kwa kocha kutokana na mipango yake ya kuibadili timu jambo lililoonekana kama kuharibu mpango mzima na kuiruhusu Tunisia itawale na hatimaye kutengeneza nafasi hadi kupata mabao mawili.
Tunisia walianza kwa kupata bao la kwanza kwa mpira wa adhabu kabla ya kupambana na kupata bao la penalti na hatimaye matokeo kuwa 3-2, matokeo ambayo ilidaiwa kwamba yalisababishwa na udhaifu kwenye eneo la ulinzi la Nigeria hali ambayo haikuonekana katika kipindi cha kwanza.
Chelle hata hivyo alitetea uamuzi wake wa kuwaingiza mawinga wawili, Chidera Ejuke na Moses Simon kwa madai kwamba hatua hiyo ilikuwa ni mbinu ya kuikabili timu ya Tunisia ambayo ilibadili mbinu za kiuchezaji.
“Ni kwa sababu walijua mbinu yetu na ndio maana nikafanya mabadiliko, unapokuwa na mawinga wawili hawawezi kwenda eneo hilo lakini walikuwa sahihi kwa sababu walitengeneza bao na kupata jingine kwa penalti,” alisema Chelle.
Chelle hata hivyo alikiri kuwapo udhaifu katika safu ya ulinzi ya timu yake kusisitiza umuhimu wa kufanya maboresho na kukabiliana na presha za dakika za lala salama.
Kocha huyo ambaye Jumatatu timu yake itaikabili Msumbiji katika hatua ya mtoano, hata hivyo alijigamba kwa kufafanua kwamba hakuna timu ambayo inaweza kukabiliana na hali ya presha ya namna ile kwa dakika 90 kama ilivyokuwa timu yake.
