Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesema kwamba haiwezekani kumpata mbadala wa kiungo na nahodha wake, Bruno Fernandes ambaye huenda akawa nje ya uwanja kwa kipindi cha mwezi mmoja baada ya kuumia.
Fernandes, 31, Jumapili iliyopita katika mechi na Aston Villa alipata matatizo ya misuli na kutolewa, mechi ambayo Man United ililala kwa mabao 2-1 na mchezaji huyo hatarajii kucheza mechi dhidi ya Newcastle itakayochezwa kesho Ijumaa Desemba 26, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Amorim hata hivyo hakuweza kuweka wazi ni muda gani hasa ambao Fernandes atakuwa nje ya uwanja akijiuguza ingawa alibainisha kuwa mchezaji huyo atakuwa nje kwa muda mrefu kidogo.
Habari za ndani hata hivyo zinadai kwamba Fernandes anaweza kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki tatu au nne na hivyo kumfanya ashindwe kuiwakilisha Man United katika mechi nne hadi tano.
Kukosekana kwa Fernandes ni pigo jingine kubwa kwa Amorim ambaye tayari katika kikosi chake anawakosa washambuliaji muhimu Amad Diallo na Bryan Mbeumo wanaoziwakilisha timu zao za taifa kwenye fainali za Afcon zinazoendelea nchini Morocco.
Kobbie Mainoo ambaye amekuwa akitajwa kwamba huenda anaweza kuwa mbadala wa Fernandes kwa sasa anasumbuliwa na matatizo ya nyonga.
“Haiwezekani kupata mbadala wa Fernandes, nimelisema hilo kwenye timu, tunahitaji kufanya mambo mazuri, kila mtu anatakiwa kuliangalia hilo, huyu mtu karibu katika kila shambulizi ndiye mwenye kuipanga timu,” alisema Amorim.
Amorim alisema Fernandes ni mchezaji ambaye analielewa kila eneo uwanjani na yuko makini na kila hatua ya mchezo na hata kocha anapofanya mabadiliko kwa kuwaingiza wachezaji wengine uwanjani ni Fernandes ambaye huwaelekeza wachezaji hao wapi wacheze.
