Rabat, Morocco.
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeanza vibaya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025) nchini Morocco kwa kuchezea kipigo cha mabao 2-1 mbele ya Nigeria au Super Eagles.
Katika mechi hiyo ya kwanza kwa timu zote iliyopigwa Jumanne hii Desemba 23, 2025 kwenye dimba la El Barid mjini Rabat, Nigeria ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Semiu Ajayi dakika ya 35.
Stars ilipambana na kusawazisha bao hilo katika dakika ya 50 kupitia kwa Charles M’Mombwa aliyeyatumia vyema makosa ya safu ya ulinzi ya Nigeria hadi kupata bao hilo lililoibua matumaini kwa mashabiki wa Tanzania.
Nigeria hata hivyo walizima matumaini ya Watanzania dakika mbili baadye walipoongeza bao la pili na la ushindi kupitia kwa Ademola Lookman na hivyo kujihakikishia ushindi katika mechi yao ya kwanza.
Stars na Nigeria zipo Kundi C na timu za Tunisia na Uganda, katika kundi hilo kila timu imebakisha mechi mbili kabla ya kujua hatma zao kama ni kuaga michuano mapema au kuendelea katika hatua inayofuata.
Stars itaumana na Uganda Jumamosi ya Desemba 27, 2025 siku ambayo pia Nigeria itaumana na Tunisia na Stars itamalizia na mechi dhidi ya Tunisia siku tatu baadaye, siku ambayo pia Uganda itacheza na Nigeria.
Akizungumza baada ya mechi, kocha wa Nigeria, Eric Chelle alisema mechi ilikuwa muhimu na kubwa kwa timu yake na anaamini ni muhimu kupata ushindi katika mechi ya kwanza.
Kwa upande wake kocha wa Stars, Miguel Gamondi alisema yaliyopita yamepita na hakuna wa kuwazuia katika kujiamini na kuipigania ndoto yao.
Kimataifa Nigeria yailaza Taifa Stars 2-1
Nigeria yailaza Taifa Stars 2-1
Read also
