Barcelona, Hispania
Mgombea nafasi ya urais katika klabu ya Barcelona, Marc Ciria amesema atafanya kila awezalo kumrudisha Lionel Messi katika klabu hiyo iwapo atashinda nafasi ya urais katika uchaguzi utakaofanyika mwakani.
Rais wa sasa wa klabu hiyo, Joan Laporta muda wake unafikia ukomo mwaka 2026 na tayari Ciria ametangaza nia ya kushindana na Laporta katika uchaguzi unaotarajia kufanyika kati ya mwezi Machi na Juni.
Messi ambaye aliondoka Barcelona au Barca mwaka 2021 na kuhamia PSG kabla ya kujiunga na Inter Miami ya Marekani kwenye ligi maarufu ya MLS, jina lake mara kadhaa liliwahi kuwa mjadala kuhusu kurudi Barca.
Awali iliaminika baada ya kumaliza mkataba PSG, Messi angerudi Barca lakini akatimkia Marekani na kuwa msaada mkubwa kwa timu yake ya Inter Miami ambayo hivi karibuni ameiongoza kubeba taji la MLS.
Katika uzinduzi wa kampeni ya kuwania urais wa klabu hiyo, Ciria alisema wanachotaka ni kuona wakongwe wao wakirudi katika klabu hiyo na hilo halifanyiki kwa siri au kwenye giza nene.
“Tutafanya kila liwezekanalo kufanikisha hilo, Messi ni mtu wa kipekee katika klabu hii, ni lazima arudi akiwa mwenye kuungwa mkono na mfumo na taratibu nzuri zilizopo, uhusiano wa Messi na Barca unatakiwa uwe kama wa Michael Jordan na Nike,” alisema Ciria.
Ciria alifafanua kwamba uhusiano huo ni lazima uende mbali kutoka katika masuala ya kibiashara hadi maeneo ya kitaasisi kwenye klabu hadi kwa wadhamini pamoja na maendeleo ya wachezaji katika La Masia (academy).
Aliongeza kuwa iwapo watawatumia wachezaji bora walio katika historia ya Barca wanaweza kufanya mambo mengi na kuingiza fedha nyingi kwa kuwa kuwarudisha nyumbani ni muhimu kama klabu itataka kushinda matatizo ya matumizi ya fedha yanayowakabili.
