Manchester, England
Klabu ya Manchester United inadaiwa kukasirishwa na kitendo cha Shirikisho la Soka Morocco (FRMF) kukataa kumruhusu Noussair Mazraoui (pichani) aichezee timu hiyo mechi dhidi ya Bournemouth iliyochezwa Jumatatu.
Man United ilipanga kuwa na mchezaji huyo katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England ambayo iliisha kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 4-4.
Mechi hiyo ya ligi ilikuwa ikichezwa siku sita kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambazo zinafanyika nchini Morocco na Man United ilikuwa na matumaini makubwa ya kuwa na Mazraoui.
Mazraoui ambaye yumo katika kikosi cha Morocco kwa ajili ya fainali hizo hakuwapo katika mechi hiyo licha ya uamuzi wa Fifa wa Desemba 3 wa kuzitaka klabu zibaki na wachezaji hadi Desemba 15 badala ya siku 14 kabla ya michuano hiyo.
Taarifa zaidi zinadai kwamba suala hilo lilifika Fifa ambao hata hivyo walizitaka klabu na mashirikisho ya soka kumaliza utata wowote utakaoibuka kwa mazungumzo yenye nia njema.
Mazraoui alionekana akifanya mazoezi na kikosi cha Man United kwa wiki yote lakini mwishowe alijiunga na kambi ya timu yake ya taifa kitendo ambacho kilionekana kuwakera Man United.
Hali hata hivyo imekuwa tofauti ya wachezaji wengine wa Afrika wanaochezea Man United kutoka Cameroon na Ivory Coast ambao walikubali kuwachelewesha wachezaji wao Bryan Mbeumo na Amad Diallo.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim awali alinukuliwa akielezea matumaini yake kwa timu za Afrika kukubali kuwachelewesha wachezaji wao ili awatumie kwa baadhi ya mechi jambo ambalo kwa Mazraoui lilishindikana.
Kimataifa Man Utd, Morocco zavuragana, kisa, Mazraoui
Man Utd, Morocco zavuragana, kisa, Mazraoui
Read also
