Na mwandishi wetu
Wachezaji wa Simba, mshambuliaji Jonathan Sowah (pichani) na kiungo, Allasante Kante wamefungiwa mechi tano kwa makosa ya utovu wa nidhamu waliyoyafanya katika mechi yao ya Ligi Kuu NBC dhidi ya Azam FC.
Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyopatikana Jumanne Desemba 16, 2025 ilieleza kuwa uamuzi huo umetokana na kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kilichofanyika Desemba 15, 2025 kutathmini matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
Katika maamuzi hayo, Sowah mbali na kufungiwa mechi tano pia ametozwa faini ya Sh milioni moja, kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha uanamichezo kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Azam, Himid Mao.
Kwa upande wa Kante ambaye kama ilivyo kwa Sowah naye ametozwa faini ya Sh milioni, katika mchezo huo huo ambao Simba ililala kwa mabao 2-0, alimpiga teke kwa makusudi mchezaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Naye mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Abdallah Mwinyimkuu wa Singida ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi katika mizunguko mitano ya ligi hiyo kwa kushindwa kutafsiri vyema sheria za soka na kutochukua hatua dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni za mchezo huo.
Kamati pia imeitoza faini ya Sh milioni tano klabu ya Yanga kwa kosa la shabiki wake kutoka jukwaani na kuvuka uzio na kwenda eneo la kuchezea wakati wa mechi yao na Coastal Union kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Akiwa uwanjani shabiki huyo alifika kwenye goli la Coastal Union kabla ya kuinama kama vile alikuwa akiweka au kuokotaa kitu katika eneo hilo jambo ambalo limetajwa kuwa ni kuhatarisha usalama wa wachezaji.
Adhabu hiyo inahusisha kanuni ya ligi kuu kuhusu udhibiti kwa klabu ingawa baadhi ya mashabiki wa soka walilihusisha tukio hilo na vitendo vya ushirikina.
Naye kiungo wa Singida Black Stars, Khalid Aucho amefungiwa mechi tano na kutozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kumsukuma na kumpiga mchezaji wa TRA United, Adam Adam, katika mechi baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC na TRA kutoka na ushindi wa mabao 3-1.
Mwamuzi wa mechi hiyo, Alex Pancras wa Dar es Salaam amepewa onyo kali kwa kushindwa kutafsiri vyema sheria za soka na kushindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya Aucho.
Soka Sowah, Kante stop mechi tano
Sowah, Kante stop mechi tano
Read also
