Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba kwa kushirikiana na Kampuni ya JayRutty imetangaza punguzo la bei ya jezi zake katika kipindi cha Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya huku wakihimiza kukataa jezi feki.
Punguzo hilo lililotangazwa Jumanne hii Desemba 16, 2025 linahusisha bei ya jezi kutoka Sh 45,000 hadi Sh 12,000 kwa jezi za ligi na kimataifa kwa jezi za watu wazima na za watoto ambazo pia zitakuwa mitaani.
Kwa mujibu wa msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally, uamuzi huo ni katika hatua ya klabu kutaka kwenda sawa na dunia inavyokwenda lakini hapo hapo wanapambana na jezi feki.
Ally alisema kwamba kama kuna wanachama wa Simba walikuwa wakinunua jezi feki kwa Sh 15,000 sasa wataipata jezi ambayo ni original yaani si feki kwa Sh 12,000.
Alisema kwamba huu ni wakati wa kuvaa jezi original na kufafanua kwamba bei ya punguzo inaanza Desemba 16, 2025 na itakwenda hadi Januari 30, 2026 muda ambao ni sawa na siku 45 kwa wateja kufaidika na ofa hiyo.
Akizungumzia upatikanaji wa jezi hizo, Ally alisema wameamua kurahisha mambo ambapo wateja wataipata kupitia mitandao ya simu kwa kulipia kupitia namba 61223807 na baada ya hapo watakwenda kwenye ofisi ya Shirika la Posta au ofisi za JayRutty.
Kwa mujibu wa Ally, mteja ataruhusisiwa kununua jezi kwa idadi yoyote anayotaka na kuchagua rangi au saizi inayompendezea wakati akifika kwenye ofisi kuchukua jezi zake.
Katika kipindi cha siku 45 za ofa hiyo, Ally alisema kwamba mteja pia anaweza kukopa na kuwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo kabla haijafika mwisho.
“Unaweza kupata jezi hata kwa kukopa, mitandao yote ya simu wanakopesha wateja, ni fursa ambayo hatupaswi kuichezea, huu ndio wakati wa kila Mwanasimba kununua jezi yake original,” alisema Ally.
