Doha, Qatar
Mshambuliaji wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa Ousmane Dembele ametangazwa kuwa mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa kwa upande wa wanaume katika tukio lililofanyika usiku wa Jumanne, Desemba 16, 2025 mjini Doha, Qatar.
Hiyo ni tuzo ya pili kubwa kwa Dembele katika kipindi kisichozidi miezi minne, baada ya mchezaji huyo kushinda tuzo ya Ballon d’Or Septemba mwaka huu.
Mafanikio ya Dembele hadi kubeba tuzo hizo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na alivyoisaidia PSG kushinda mataji manne katika msimu uliopita wa 2024-25 akiwa amehusika katika mabao 51 kwenye mechi 53 za PSG.
Katika mataji hayo limo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo PSG ililibeba kwa mara ya kwanza baada ya kuhaha kwa misimu kadhaa ikiwamo licha ya kuwa na kikosi kilichosheheni mastaa wakiwamo Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappe.
Dembele, 28, ambaye aliwahi kuichezea Borussia Dortmud kabla ya kujiunga na PSG mwaka 2023 akitokea Barca, mwaka 2023, atika tuzo hiyo ya Fifa aliwashinda Lamine Yamal wa Barca na Mbappe wa Real Madrid.
Katika makabidhiano ya tuzo hiyo, Dembele alishiriki katika hafla hiyo ambayo itafuatiwa na mechi ya taji la mabara ambapo PSG itaumana na Flamengo ya Brazil siku ya Jumatano.
Tuzo hiyo ya Fifa ambayo inahusisha matukio yaliyoanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025, mshindi hupatikana kwa njia ya kura ambazo zinapigwa na makocha wa timu za taifa, manahodha, waandishi wa habari na mashabiki.
Bonmati kinara wa wanawake
Naye kiungo wa timu ya wanawake ya Barcelona, Aitana Bonmati (pichani chini) ametwaa tuzo kama ya Dembele kwenye soka la wanawake hii ikiwa ni mara yake ya tatu kubeba tuzo hiyo, wakati kocha wa timu ya wanawake ya England, Sarina Wiegman akibeba tuzo ya kocha bora kwa mara ya tano.

Bonmati, 27, pia alikuwa mchezaji muhimu wa timu ya taifa ya wanawake ya Hispania iliyoshika nafasi ya pili katika fainali za wanawake za Euro 2025 ambazo England ilibeba taji.
Mafanikio ya Bonmati kwa kiasi kikubwa yamebebwa na mataji matatu aliyoisaidia timu ya wanawake ya Barcelona kuyabeba akifunga mabao 12 lakini pia timu hiyo ilishika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa na timu ya wanawake ya Arsenal.
Wakati huo huo kocha wa PSG, Luis Enrique, 55, ametwaa tuzo ya kocha wa mwaka baada ya kuiwezesha kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiweka rekodi kwa kuziangusha Liverpool, Arsenal na Inter Milan.
Enrique ambaye amekuwa kocha wa PSG tangu mwaka 2023 akitokea Barca, katika kinyang’anyiro cha tuzo hiyo amewashinda, Arne Slot wa Liverpool na Hansi Flick wa Barca.
Enrique hata hivyo hakuweza kushiriki katika hafla hiyo mjini Doha na badala yake kocha msaidizi wa PSG, Rafel Pol Cabanellas aliipokea tuzo hiyo kwa niaba yake.
Wachezaji 11 bora pia wametajwa katika timu bora ya mwaka, majina na klabu wanaoztoka katika mabano ni kama ifuatavyo: Gianluigi Donnarumma (PSG/Man City), Achraf Hakimi (PSG), Willian Pacho (PSG), Virgil van Dijk (Liverpool), Nuno Mendes (PSG), Cole Palmer (Chelsea), Jude Bellingham (Real Madrid), Vitinha (PSG), Pedri (Barca), Lamine Yamal (Barca) na Dembele (PSG).
