Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso amepongeza kuwapo kwa umoja katika timu yake baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Alaves katika mechi ya La Liga iliyopigwa jana Jumapili Desemba 14, 2025.
Alonso anapitia kipindi kigumu ndani ya timu hiyo kutokana na matokeo mabaya ya hivi karibuni kikiwamo kipigo cha mabao 2-1 mbele ya Man City katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kylian Mbappe, mshambuliaji aliyekuwa majeruhi aliifungia Madrid bao la kwanza, Alaves waliokuwa nyumbani wakasawazisha kupitia Carlos Vicente kabla ya Rodrygo kuipatia Madrid bao la pili kwa pasi ya Vinicius Junior.
Ushindi huo mbali na kumpa ahueni Alonso aliyekuwa akihusishwa na mipango ya kutimuliwa pia umeifanya Madrid kuwasogelea mahasimu wao Barca wanaoshika usukani katika La Liga kwa kupunguza idadi ya pointi kufikia nne.
Matokeo mabaya ya Real Madrid kwenye La Liga hususan kipigo cha mabao 2-0 mbele ya Celta Vigo yalianza kuibua hisia za kuitoa timu hiyo kwenye mbio za kusaka taji la La Liga huku kukiwa na habari kwamba mabosi walianza kuijadili nafasi ya Alonso.
Sambamba na matokeo mabaya, Alonso pia alianza kujadiliwa kuhusu uhusiano wake na wachezaji mastaa mmojawao akiwa Vinicius tangu mchezaji huyo aoneshe hasira za waziwazi baada ya kocha kumtaka aende benchi katika mechi dhidi ya Barca maarufu Clasico.
“Sisi sote tupo pamoja, tunapambana pamoja katika hatua nzuri na huu ni wakati mzuri, timu ilipambana vizuri na kwa mara nyingine tuko tayari kusonga mbele, umoja ni kitu muhimu,” alisema Alonso baada ya ushindi dhidi ya Alaves.
Kabla ya mapumziko ya Krismasi, Madrid watacheza mechi mbili ambazo pia zitakuwa kipimo kingine muhimu kwa Alonso, keshokutwa Jumatano wataumana na Talavera de la Reina katika Copa del Rey na mwishoni mwa wiki watakuwa na kibarua mbele ya Sevilla katika La Liga.
