Hassan Kingu
Simba haipo vizuri, mwenendo wa timu kiujumla hauridhishi, utata ulianza kuonekana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya timu hiyo kupoteza mechi mbili za hatua ya makundi.
Kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Azam FC, tena mabao ya jioni ni jambo jingine lililoongeza machungu na hasira za mashabiki ambao msimu uliopita waliishuhudia timu yao ikifikia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Matarajio ya msimu huu yalikuwa juu, yalianza kuzungumzwa wakati wa usajili, imani ikajengeka timu itafanya vizuri kwenye Ligi Kuu NBC na Ligi ya Mabingwa lakini matumaini yanafifia siku hadi siku.
Katika kupambana kuweka mambo sawa, Simba imeanza au inaendelea kumsaka mchawi wake, mchawi wa siku zote alikuwa Murtaza Mangungu, mwenyekiti wa klabu hiyo, na sasa mchawi mwingine ni kocha Suleiman Matola.
Ingekuwa miaka ya nyuma Mangungu angekuwa tayari ameondolewa kupitia mkutano mkuu lakini zama hizi jambo hilo ni ngumu na huenda lisipate baraka za mamlaka.
Kwa hiyo Mangungu amepenya kwenye mkutano mkuu wa hivi karibuni, licha ya kusakamwa na kuwekwa katika hali tete lakini alikuwa makini dhidi ya jaribio lolote la kumuondoa na mwisho wa siku akamaliza mkutano kimtindo.
Kuhusu suala la Mangungu kilichobaki sasa ni mkutano wa uchaguzi, hapo ndipo atakapoondolewa kupitia kura za wanachama, tofauti na hivyo kuondoka kwake kunabaki kuwa jambo gumu.
Walioamini mkutano ungemng’oa Mangungu wamefeli wasubiri kura na kwenye kura ni kama ataamua kukaa kando vinginevyo ni vigumu kutabiri kama atashinda au atashindwa, hilo litategemea mengi ikiwamo aina ya wapinzani atakaokutana nao au mwenyewe kujiweka kando au kuwekwa kando na katiba.
Kuhusu Matola ambaye naye anatajwa na kuhusishwa na mwenendo mbaya wa Simba hasa baada ya timu hiyo kufungwa na Azam yeye ni tofauti na Mangungu, Matola anaweza kuondoka au kuondolewa wakati wowote.

Uamuzi dhidi ya Matola unahusisha watu wachache na ndio maana imekuwa rahisi kusikia watu kwenye mitandao wakimjadili katika namna mbaya na wengine kudiriki kusema kwamba siku zake ndani ya Simba zinahesabika.
Majina haya mawili kwa siku za karibuni yamekuwa yakitajwa sana hasa mitandaoni wakinangwa na kuonekana ndio msingi wa tatizo ndani ya Simba.
Kwa hali ilivyo mitandaoni kama kuna mtu labda ni mgeni na mambo ya soka la Tanzania na hajui kinachoendelea anaweza kujiambia kwamba ni kwa nini watu hao wawili hawaondoki ili Simba iwe bora.
Kwa upande mwingine napata tabu kuamini kuwa Matola na Mangungu pekee ndio tatizo la Simba badala yake naona kuna mambo muhimu kuyafanyia tafakuri na kuyapatia majibu badala ya kuwajadili na kuwasakama watu hao wawili.
Hao watu wawili wanaotajwa msimu uliopita walikuwa Simba iliyofikia fainali Kombe la Shirikisho Afrika huku matumaini yakiwa juu kwamba timu hiyo ilikuwa na uwezo wa kuweka historia kwa kubeba taji hilo.
Kilichotarajiwa ni kwamba Simba iliyofikia fainali Shirikisho Afrika msimu uliopita ingeendeleza mafanikio msimu huu lakini dalili za jambo hilo hazionekani.
Nionavyo kabla ya kuanza na Mangungu au Matola ambao walikuwa na timu hiyo msimu uliopita ni vyema kujiuliza kuhusu usajili, je timu ya msimu uliopita na hii ya sasa ipi bora?
Hili ni swali au hoja ngumu na ya kiufundi ambayo inahitaji tafakuri kabla ya kuijibu na ndio maana wengi hatuitaki badala yake yanatafutwa maswali au hoja rahisi yenye majibu rahisi kama vile Mangungu tatizo na sasa Matola tatizo.
Baada ya kikosi hoja au swali la pili kwangu ni kuhusu kocha, je Simba wana mpango gani katika kupata kocha mwenye hadhi au uwezo unaolingana na ule wa Fadlu Davids ambaye aliifikisha timu hiyo fainali ya Shirikisho Afrika?.
Fadlu si tu aliifikisha timu fainali bali hata aina ya soka lake ilivutia na ni sababu kubwa ya kuwapo matumaini kwamba Simba ya msimu huu ingekuwa moto chini ya kocha huyo lakini hali imekuwa tofauti, Fadlu ameondoka wakati anahitajika.
Kwa mantiki hiyo badala ya Mangungu na Matola, tafakuri au swali ambalo wana Simba wanapaswa kujiuliza na kutafuta majibu iwe katika hayo mambo mawili, kwanza kikosi na pili kuhusu kocha wa hadhi ya Fadlu.
Kinyume na hapo kwangu naona ni sawa na kujiuliza swali rahisi na kujipa jibu rahisi ambalo katu haliwezi kuisaidia timu.
