Washington, Marekani
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka wa Fifa, Arsene Wenger ametetea uamuzi wa ongezeko la idadi ya timu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 kufikia 48 akisema hiyo ni idadi sahihi kwa fainali hizo.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika katika nchi za Canada, Marekani na Mexico zitakuwa za kwanza kushirikisha timu 48 kutoka michuano saba iliyopita ambayo ilishirikisha timu 32.
Uamuzi wa kuongeza timu hadi 48 umeibua hofu juu ya uwezekano wa kupoteza ushindani, ubora na hadhi ya fainali hizo lakini Wenger ambaye ni kocha wa zamani wa Arsenal ametetea ongezeko la timu.
Akizungumza mbele ya jopo la maofisa wa Fifa akiwamo kocha wa zamani wa timu ya wanawake ya Marekani, Jill Ellis, kabla ya droo ya fainali hizo, Wenger alisisitiza kuwa timu 48 ni sahihi.
“Naamini timu 48 ni sahihi, ni chini ya asilimia 25 ya nchi 211 wanachama wa Fifa, maana yake ni kwamba timu moja kati ya nne ina nafasi ya kushiriki, pia asilimia 75 ya timu hazitakuwamo,” alisema Wenger.
Kuhusu uwezekano wa ubora wa mashindano kupotea, Wenger alitolea mfano wa michuano ya hivi karibuni ya Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 17, michuano ambayo pia ilishirikisha timu 48.
Wenger alisema anaamini katika ubora kwa sababu ili ufuzu ni lazima ushinde timu katika bara lako na hiyo ni ishara ya ubora, ni suala la kupata matokeo.
Alisema kwamba swali kuhusu ubora liliulizwa hata kwenye michuano ya vijana chini ya miaka 17 lakini matokeo yake ni kwamba walikutana na ubora uliowashangaza.
“Timu hazimo kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa sababu zipo tu zimealikwa, hapana ni kwa sababu zimepata ushindi dhidi ya timu nyingine katika bara lao, suala la ubora linaonekana, angalia playoffs, aina ya wachezaji na aina ya timu zinazocheza,” alisema Wenger.
