Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba imefikia makubaliano ya kuachana na meneja wake, Dimitar Pantev ikiwa ni takriban miezi miwili imetimia tangu wamkabidhi jukumu hilo.
Pantev alitangazwa rasmi na klabu ya Simba Oktoba 4 mwaka huu akichukua nafasi ya Fadlu Davids lakini taarifa ya klabu hiyo ya Desemba 2, 2025 ilitangaza kuachana na kocha huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Simba na Pantev walifikia makubaliano hayo na sasa timu hiyo itakuwa chini ya Suleiman Matola ambaye ni kocha msaidizi.
Katika taarifa ya kuingia mkataba na Pantev ambaye anatokea Bulgaria, klabu ya Simba ilieleza katika taarifa yake kuwa Pantev atakuwa meneja hali ambayo ilizua mjadala kwa baadhi ya mashabiki wa soka.
Katika mjadala huo mashabiki walikuwa wakihoji kama kweli Pantev ni meneja au kocha mkuu au Simba imekuja na utaratibu mpya ingawa kwa wengi alionekana akifanya majukumu ya kocha uwanjani.
Pantev anaiacha Simba ikiwa na mwendelezo mzuri kwenye Ligi Kuu NBC ingawa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo tayari imepoteza mechi mbili kati ya sita za hatua ya makundi.
Soka Simba yamtema Pantev
Simba yamtema Pantev
Read also
