Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso amesisitiza kuwa anaendelea kuungwa mkono na wachezaji wake na yuko katika hali ya utulivu wakati huu zikiwapo habari kwamba kibarua chake kipo njia panda.
Madrid itaumana na Man City Jumatano hii Novemba 10, 2025, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ambayo matokeo mabaya kwa timu hiyo huenda yakawa sababu tosha ya kutimuliwa kwa Alonso.
Mwenendo wa Madrid katika mechi za karibuni si mzuri, timu hiyo imeshinda mechi moja kati ya tano zilizopita ikiwamo Jumapili ilipolala kwa mabao 2-0 mbele ya Celta Vigo hali ambayo ilizidisha presha kwa Alonso.
Habari zaidi zinadai kwamba baada ya matokeo dhidi ya Celta Vigo, rais wa klabu hiyo, Florentino Pérez alifanya kikao na wajumbe wa bodi kujadili mwelekeo wa Alonso kukiwa na hofu kuhusu uongozi wake na viwango vya wachezaji tegemeo wa timu hiyo.
Kwa upande wake Alonso alipoulizwa na waandishi wa habari iwapo anaungwa mkono na wachezaji wake, kocha huyo alijibu, ndiyo na kufafanua kuwa kuna umoja katika kikosi chake.
“Timu ipo katika hali ya umoja, inashawishi, kila mmoja anaamini tutashinda kesho (Jumatano) hakuna mwenye shaka lakini katika hilo ni lazima tucheze kwa mwenendo mzuri, tuwe imara na washindani,” alisema Alonso.
Naye kiungo wa Madrid, Aurélien Tchouameni alipozungumza baadaye alisema matokeo mabaya ikiwamo kufungwa bao 1-0 na Liverpool katika ligi ya mabingwa na sare tatu dhidi ya Rayo Vallecano, Elche na Girona kabla ya kupoteza mbele ya Celta Vigo, tatizo si Alonso.
Tchouameni alifafanua kuwa katika mechi na Celta Vigo, kocha alikuwa na mpango mzuri lakini mwisho wa siku ni wao wachezaji ndio wanaokuwa uwanjani kama wakiwa katika kiwango chao wanakuwa na nafasi nzuri ya kushinda na wakipoteza kunakuwa na tatizo baina yao uwanjani na si kocha.
