London, England
Mshambuliaji wa Cheslea, Cole Palmer yuko fiti kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu England kesho Jumapili Novemba 30, 2025, dhidi ya mahasimu wao wa London, Arsenal, mechi itakayopigwa Stamford Bridge.
Palmer (pichani) mwenye umri wa miaka 23 alikuwa na matatizo ya kidole gumba tangu wiki iliyopita na hivyo kukosa mechi mbili ambazo timu yake imeshinda dhidi ya Burnley na Barcelona.
Kwa ujumla msimu huu haujawa mzuri kwa Palmer ambaye amekuwa akiandamwa na janga la kuwa majeruhi akicheza mechi tano tu za mashindano yote hadi sasa.
Kwa mujibu wa kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, mchezaji huyo yuko fiti na anaweza kuanza mechi hiyo jambo ambalo kila mtu katika klabu huyo analifurahia.
“Kila mmoja ana furaha, kuanzia wachezaji wenzake, sote tuna furaha na jambo la muhimu zaidi ni kwamba Cole (Palmer) ana furaha kwa sababu mwanasoka yeyote anataka kucheza mechi na kuwa sehemu ya timu kila siku,” alisema Maresca.
Maresca alisema kwamba Palmer ni mchezaji wao mzuri na wana furaha amerudi kwenye timu huku akimtaka kujitoa kwa asilimia 100 na tayari amefanya makubwa siku za nyuma na hakuna shaka kwamba atakuwa mwenye kuifanyia klabu makubwa siku zijazo.
Kukosekana kwa Palmer ni pigo kubwa kwa Chelsea ambao katika Ligi Kuu England wanashika nafasi ya pili nyuma ya vinara Arsenal na wanaweza kupunguza tofauti ya pointi hadi tatu iwapo watashinda mechi ya Jumapili.
