London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema anaamini kuna mengi mazuri yanakuja kutoka kwa kiungo Declan Rice kuelekea mechi ya Jumapili dhidi ya Chelsea, timu yenye wachezaji mahiri, Enzo Fernández na Moisés Caicedo.
Wachezaji hao watatu thamani yao inatajwa kufikia Dola 396 milioni na wanatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora katika Ligi Kuu England kwa msimu huu.
Wiki hii Rice (pichani juu) alikiri kumpigia kura Caicedo katika timu yake bora ya mwaka kwa msimu wa 2024-25 wakati mjadala kuhusu mchezaji bora wa ligi hiyo ukipamba moto.
Arteta amesisitiza kuwa pamoja na kiwango cha juu anachoendelea kuonesha Rice bila kushuka, kocha huyo amemtaka Rice ambaye pia ni mchezaji wa kimataifa wa England kujitahidi ili kiwango kiwe juu zaidi.
Alipoulizwa kama Rice yuko katika ubora unaotakiwa, Arteta alijibu ndio akizingatia miaka miwili au mitatu iliyopita lakini kwa sasa kwa kuwa yuko naye kila siku na anajihusisha naye kwa yanayoendelea, anaamini atawapa mengi zaidi.
“
Ni kwa sababu anataka zaidi, timu inamjua vizuri, jukumu lake kwenye timu linazidi kukua, matokeo ya kazi yake kwenye timu ni makubwa,” alisema Arteta.
Arteta alisema kwamba alimjua Rice kwa muda mrefu kabla ya kusajiliwa Arsenal na alijua namna atakavyokuwa sehemu ya timu na kuhusika katika mabadiliko kwenye timu na tayari amefanya yote ana ataendelea kufikia matarajio.
Alipoulizwa kuhusu mechi iliyomfanya ashawishike kumsajili Rice, Arteta alisema kwamba hakumbuki mechi yoyote lakini anachojua ni kwamba mchezaji huyo alikuwa kwenye fikra zake.
