Madrid, Hispania
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Hispania, Luis de la Fuente amepuuza habari ya kuwapo tofauti kati yake na klabu ya Barcelona kuhusu klabu hiyo inavyomtumia winga wao Lamine Yamal.
Badala yake De la Fuente amesisitiza kuwa mawasiliano baina yake na klabu ya Barcelona au Barca yanahitaji kuwa katika namna iliyo bora zaidi.
Jumanne iliyopita Shirikisho la Soka Hispania lilitoa taarifa likielezea kushangazwa kwake baada ya kubaini kuwa winga huyo mwenye miaka 18 yuko katika taratibu za matibabu bila ya klabu yake kuarifiwa mapema.
Akizungumzia hilo De la Fuente alisema mahusiano na klabu zote yapo vizuri ingawa kila kitu kinahitaji kuboreshwa licha ya ukweli kwamba kimsingi mambo yanakwenda vizuri.
“Habari nzuri ni kwamba (Yamal) mchezaji huyo bado ana miaka 15 zaidi ya kuendelea kuichezea timu ya Hispania, ni lazima tuyafirikie ya sasa na ya baadaye,” alisema De la Fuente.
De la Fuente alisema mtazamo wao kwa wakati huu ni kuangalia namna ya kuwategemea wachezaji waliopo na kufuzu, vinginevyo kila kitu kitaendelea kuboreshwa ingawa wanafanya vizuri na wataendelea kufanya vizuri.
Hispania chini ya De La Fuente inakwenda vizuri katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 ikiwa imeshinda mechi zote nne bila ya kufungwa na ushindi dhidi ya Georgia utaweka rekodi kwa timu hiyo kucheza mechi 30 bila kupoteza.
De la Fuente hata hivyo alisema kwa wakati huu hawaangalii rekodi nzuri za timu yake badala yake wanachotaka ni kushinda mechi na Georgia na kufuzu Kombe la Dunia.
