Na mwandishi wetu
Simba imetoka kifua mbele kwenye dimba la Meja Jenerali Isamuhyo baada ya kuitandika JKT Tanzania mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa Jumamosi Novemba 8, 2025.
Timu zote zilikianza kipindi cha kwanza kwa kusomana na kufanya mashambulizi ya hapa na pale lakini hadi dakika 45 zinakamilika hakuna timu iliyoliona lango la mwenzake.
JKT ndio waliokuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Simba kwa bao la Edward Songo, lililopatikana katika dakika ya 60 ya mchezo huo kwa shuti la mbali lililomshinda kipa Yakoub Suleiman ambaye ni kipa wa zamani wa JKT.
Iliwachukua dakika zisizozidi tatu sIMBA kusawazisha bao hilo na aliyesawazisha bao ni Wilson Nangu, beki wa zamani wa JKT ambaye kama ilivyo kwa Suleiman naye alicheza dhidi ya waajiri wake wa zamani na ndiye aliyetajwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Bao la ushindi la Simba lilipatikana dakika ya 77 mfungaji akiwa Jonathan Sowah, nyota wa zamani wa Singida Black Stars ambaye hilo linakuwa bao lake la pili kwenye ligi msimu huu.
Kwa ushindi huo Simba sasa inashika usukani wa ligi hiyo ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zake tatu ilizocheza hadi sasa.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Pamba FC ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ilitoka sare ya bao 1-1 na Singida Black Stars, bao la Singida BS lilifungwa na Clatous Chama dakika ya 31 na Pamba kusawazisha dakika ya 51 kwa bao la Kelvin Nashon ambaye ni mchezaji wa zamani wa Singida BS.
Pamba baada ya matokeo hayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa kama Simba lakini Pamba imezidiwa kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Soka Simba yaitandika JKT Tanzania 2-1
Simba yaitandika JKT Tanzania 2-1
Read also
