Lubumbashi, DR Congo
Klabu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imethibitisha mmoja wa mashabiki wake kuuawa Jumapili iliyopita wakati wa mechi na mahasimu wao FC Lupopo baada ya kuchomwa na kisu.
Taarifa ya TP Mazembe iliyopatikana Jumatatu Novemba 3, 2025 ilithibitisha kifo cha shabiki huyo ambacho kilitokea wakati wa mechi hiyo mjini Lubumbashi katika kitongoji cha Kenya.
TP Mazembe ambao ni mabingwa mara tano wa Afrika, katika taarifa yao, walielezea masikitiko yao kutokana na kifo cha shabiki huyo kilichotokea kwenye Uwanja wa Frederic Kibassa-Maliba.
Katika tukio hilo shabiki huyo alichomwa kisu kichwani na ingawa alikimbizwa katika kituo kidogo cha afya karibu na uwanja huo lakini majeraha yalikuwa makubwa na ndipo alipohamishiwa katika Hospitali ya Kenya akiwa tayari amefariki.
Taarifa ya TP Mazembe ililaani tukio hilo la uhalifu ambalo ni kinyume na maadili ya michezo na kutaka mamlaka husika kufanya uchunguzi na kuweka kila kitu wazi kuhusiana na kitendo hicho cha kusikitisha.
Rais wa TP Mazembe ambaye pia ni mfanyabiashara na mwanasiasa, Moise Katumbi alielezea kusikitishwa kwake na tukio hilo na kutuma salamu za pole kwa famlia ya marehemu na jamii yote ya watu wa TP Mazembe.
Katika mechi hiyo, FC Lupopo walitoka na ushindi baada ya kuwa nyuma kwa bao 1-0, walisawazisha na kuongeza bao la pili dakika ya 87 lililofungwa na Ravel Djoumekou na kufanya ubao wa matokeo usome 2-1.
Bao hilo la pili liliibua shangwe kwa mashabiki wa FC Lupopo waliokuwa nyumbani kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 20,000 huku mashabiki wa TP Mazembe wakipambana wao kwa wao na wengine kuharibu mali za uwanja na kurusha baadhi ya vitu hivyo uwanjani.
Kimataifa Shabiki TP Mazembe auawa kwa kisu
Shabiki TP Mazembe auawa kwa kisu
Read also
