Na Hassan Kingu
Klabu ya Simba inaonekana imedhamiria kuikataa kwa nguvu zote biashara ya jezi feki, ni kama vile klabu hiyo imeamua kuanzisha vita dhidi ya wanaosambaza na kuuza jezi hizo ambazo zinawanyima mapato.
Ni hatua ya kupongezwa lakini hapo hapo ni muhimu kutambua ukweli kwamba vita au mapambano ya aina hii hayajawahi kuwa kitu rahisi si Tanzania tu bali hata kwingineko Afrika au duniani kwa ujumla.
Biashara ya jezi feki ni kubwa, ni aina ya biashara ambayo baadhi ya watu wanajaribu kuihalalisha na wameihalalisha kwa namna ambavyo wamekuwa wakiifanya kwa muda mrefu bila kujali.
Sababu mojawapo inayowafanya watu hawa kuihalalisha biashara hii ni ukweli kwamba wanaoibiwa wanatumia nguvu ndogo au hawajaonesha utayari wa kupambana nao kwa kutumia nguvu kubwa.
Klabu ya Simba kwa kushirikiana na wadhamini wao Kampuni ya Jayrutty hadi sasa wameonesha dalili zote za utayari na kufanya kila linalowezekana kukabiliana na uuzwaji na usambazaji wa jezi feki.
Hata hivyo kama nilivyosema awali ni muhimu kutambua ukweli kwamba Simba peke yao bado hawatoshi kumaliza tatizo hili bali klabu zote kuanzia mahasimu wao Yanga na klabu nyingine za ligi kuu ni muhimu kushiriki kwa pamoja katika vita hii.
Ukweli kwamba kuna watu wamejihalalishia biashara hii na wana nguvu za kiuchumi ndio unaonifanya niamini kuwa klabu zote hasa za ligi kuu pamoja na wadau wa soka wana kila sababu ya kushiriki katika vita hii.

Mafanikio ya vita hii ni mafanikio ya michezo, ni mafanikio ya soka, serikali na jamii ya watanzania kwa kuwa sehemu kubwa ya jezi feki huwa hazilipiwi kodi.
Kwa hali hiyo unapopiga vita jezi feki unakuwa umepambana katika kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi lakini la muhimu zaidi ni kwamba unasaidia maendeleo ya klabu kiuchumi na soka kwa ujumla wake.
Ikumbukwe kwamba wanaouza jezi kihalali ni wanamichezo hivyo wana nafasi pia ya kuunga mkono michezo mingine kadri wanavyopata faida na faida yao itapatikana zaidi jezi feki zikidhibitiwa.
Na hapa ndipo tunapouona ukweli kwamba vita ya jezi feki si sahihi kuwa ya Simba na washirika wao yaani Jayrutty badala yake ni vita ya wanamichezo, watanzania na wote wanaopenda haki.
Kama nilivyosema kwamba kuna kundi kubwa la watu ambao limejihalalishia biashara hii kwa imani kwamba wana haki ya kununua jezi na kuzitengeneza upya chini ya ubora na kuziuza kwa faida wakati mwingine faida kubwa kuliko klabu husika au mdhamini.
Hili si jambo sahihi kibiashara na katika misingi ya haki halikubaliki na ndio maana nasisitiza kwa klabu zote kusimama kidete katika vita hii.
Simba wameanza ni vyema kwa namna ambavyo wanafanya kampeni zao mikoani zenye lengo la kukataa jezi feki, juhudi zao ni vyema zikiungwa mkono, peke yao vita hii ni ngumu na inawapa nguvu wanaoifanya kuona kwamba wanapambana na nguvu ndogo kwa maana ya Simba peke yao.
Na ndio maana nasisitiza tena na tena kwamba wadau wote wa soka kwa pamoja kuanzia klabu, TFF, serikali na wengineo nguvu yao inahitajika katika hiki kinachofanywa na Simba kwa kushirikiana na Jayrutty.
Kinachoonekana sasa mbele ya wengi ni kama vile jukumu la kuzikataa jezi feki ni la ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally na kundi lao la Simba kwa kushirikiana na Jayrutty au waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ambaye hivi karibuni ameonekana kuunga mkono juhudi hizo wakati si kweli.
Ni muhimu nguvu iongezeke, wadau washirikiane kwa pamoja kuwakumbusha watanzania kuthamini na kuheshimu hakimiliki kwa maana ya kwamba wenye haki ya kuuza jezi ya Simba ni watu maalum kwa makubaliano maalum na si kila mtu.
