Na mwandishi wetu
Kocha mkuu mpya wa Yanga, Pedro Gonçalves, ameanza na ushindi baada ya timu yake kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa Jumanne, Oktoba 28, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Kinondoni, Dar es Salaam.
Gonçalves ameanza kibarua hicho baada ya kutimuliwa kwa Romain Folz, kocha aliyeiongoza timu hiyo kwenye igi kwa ushindi wa mechi dhidi ya Pamba na sare ya bila kufungana na Mbeya City kabla ya kutimuliwa.
Iliwachukua Yanga dakika 39 kuandika bao lao la kwanza mfungaji akiwa beki na nahodha wa zamani wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Junior’ kwa shuti alilolipiga akiwa nje kidogo ya eneo la 18.
Jitihada za kipa wa Mtibwa, Constantine Malimi kuuzuia mpira huo hazikufanikiwa badala yake alishtukia mpira ukimzidi na kujaa wavuni.
Yanga waliendelea kulisakama lango la Mtibwa lakini umakini wa safu ya ulinzi ulikuwa kikwazo na hadi dakika 45 za awali zinakamilika Yanga walibaki na bao lao moja.
Kipindi cha pili timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini walikuwa ni Yanga waliopata bao la pili dakika ya 83, bao lililofungwa na Ecua ambaye aliingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Edmund John.
Katika hatua nyingine mashabiki wa Yanga walionekana kumpa sapoti mshambuliaji wao Prince Dube ambaye anapitia kipindi kigumu kwa namna ambavyo amekuwa akipoteza nafasi nyingi za kufunga.
Pamba yapewa pointi tatu
Wakati huo huo timu ya Pamba ya Mwanza imepewa pointi tatu na mabao matatu ya bure baada ya mechi yao na Dodoma Jiji kuvunjika kabla ya wakati kutokana na tatizo la taa uwanjani.
Pamba waliokuwa ugenini mjini Dodoma wamepewa pointi hizo na kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), uamuzi ambao umetangazwa Jumanne hii na Idara ya Habari ya TPLB.
Katika taarifa ya TPLB ilielezwa kuwa Dodoma Jiji ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo walishindwa kuandaa mchezo kikamilifu na kusababisha mchezo kuvurugika kabla ya kuvunjwa kwa mujibu wa kanuni.
Soka Kocha mpya Yanga aanza na ushindi
Kocha mpya Yanga aanza na ushindi
Read also
