Madrid, Hispania
Real Madrid imetoka kifua mbele dhidi ya mahasimu wao Barcelona kwa kuwachapa mabao 2-1, leo Jumapili Oktoba 26, 2025, mechi ambayo baada ya dakika 90 ilitawaliwa na mzozo wa wachezaji Lamine Yamal na Vinicius Junior au Vini Jr.
Real Madrid wakiwa nyumbani Santiago Bernabeu, walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Kylian Mbappe kwa pasi ya Jude Bellingham ambaye aliivuruga safu ya ulinzi ya Barca kabla ya kutoa pasi iliyozaa bao hilo.
Barca walikuja juu na kusawazisha bao hilo dakika ya 38 kwa bao la FermÃn López ambaye aliitumia pasi ya Marcus Rashford, mshambuliaji wa Man United anayeichezea Barca kwa mkopo.
Dakika mbili kabla ya mapumziko, Jude Bellingham aliipatia Real bao la pili na la ushindi baada ya kuinasa pasi ya Éder Milita.
Real walionesha kila dalili za kutoka na ushindi katika mechi hiyo, dakika ya pili tu ya mchezo, Vini Jr aliangushwa ndani ya eneo la penalti na mwamuzi kuipa Real penalti lakini ilifutwa baada ya mapitio ya VAR.
Picha ya VAR ilibaini kwamba kabla ya kuanguka, Vini Jr alimkwatua Lamine Yamal mgunni na hivyo maamuzi hayo kubadilishwa.
Ushindi huo ni hatua nzuri kwa Real kwani ni kama vile imefuta uteja baada ya kufungwa na Barca katika mechi zote nne za msimu uliopita.
Nje ya matokeo hayo ambayo yanaifanya Real kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa La Liga, tukio la Yamal na Vini Jr limeendelea kuteka hisia za mashabiki wa timu hizo mbili.
Tukio hilo lililotokea baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo liliibuka kwa kinachoaminika kuwa ni vita ya maneno baina ya wachezaji hao tegemeo kwa timu zote.

Awali mzozo ulianza kati ya Yamal na Dani Carvajal kubadilishana kauli za hasira lakini wakati Yamal akielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, Vini Jr ni kama aliuwasha moto upya kwa kumvaa Yamal kwa maneno.
Vini alianza kwa kumwambia Yamal kuwa ni mchezaji mwenye kutoa pasi za kisigino tu kabla ya kuongeza kwa kumwambia kuwa anaongea sana na kumtaka aongee baada ya matokeo hayo.
Kauli ya Vini Jr inaaminika kutokana na alichokisema Yamal kabla ya mechi hiyo kwamba Real wana tabia ya kufanya matukio ya kudanganya katika mechi zao.
Kauli za Yamal ni kama vile zilipuuzwa na wachezaji wa Real ingawa hali ilikuwa tofauti kwa mashabiki ambao kwa muda mwingi walikuwa wakimzomea mchezaji huyo.
