Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Arne Slot amesisitiza kuwa ukame wa mabao unaomkabili mshambuliaji wake Mohamed Salah ni jambo la mwisho kabisa kati ya mambo yanayoweza kumfanya awe mwenye wasiwasi.
Salah au Mo, mmoja wa washambuliaji tegemeo wa Liverpool, msimu huu amekuwa na wakati mgumu kuzifumania nyavu akiwa hadi sasa na mechi sita zilizopita bila ya bao na anaonekana kama amepoteza ubora uliozoeleka.
Msimu huu Salah ana mabao matatu hadi sasa na moja kati ya hayo amefunga kwa penalti na Jumatano iliyopita kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Eintracht Frankfurt ambayo Liverpool ilishinda, Salah alijikuta akicheza kwa dakika 16 za mwisho.
Ushindi huo dhidi ya Eintracht Frankfurt umekuwa faraja kubwa kwa timu hiyo baada ya kupitia kipindi kigumu cha matokeo mabaya hali ambayo pia imechangia kuwapo mjadala kuhusu Salah na ukame wake wa mabao na jinsi mshambuliaji huyo anavyopoteza nafasi za kufunga ingawa Slot hana wasiwasi katika hilo.
“Sijui kama ni kasi imepungua au la, ni jambo gumu, naweza kuja na sababu kadhaa ambazo pia sina uhakika kama ni sahihi, kwa ujumla wachezaji huwa wanapoteza nafasi na Mo pia ni binadamu, hatujamzowea kupoteza nafasi licha ya nafasi hizo kuwa nyingi kwa sasa tena mfululizo lakini haya mambo hutokea,” alisema Slot.
Jumamosi hii Liverpool itajitupa uwanjani kukabiliana na Brentford na bila shaka Slot na Salah wanaimani kwamba mechi hiyo inaweza kuwa mwanzo mpya kwa mshambuliaji huyo.
