Na mwandishi wetu
Beki na nahodha wa Simba, Shomari Kapombe amechaguliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwaka 2025 (Inter club) ambapo atachuana na mshambuliaji wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anaichezea Pyramids ya Misri, Fiston Mayele.
Mbali na Mayele na Kapombe wachezaji wengine ambao majina yao yamo kwenye orodha ya CAF wakiwania tuzo hiyo ni Ahmed Samy (Pyramids), Emam Ashour (Al Ahly), Ibrahim Adel (Pyramids), Mohamed Hrimat (AS FAR), Mohamed Chibi (Pyramids) na Oussama Lamlioui (RS Berkane).
Wengine watakaochuana na Kapombe katika kipengele hicho ni Ismael Belkacemi (Al Ahli Tripoli), Blati Toure (Pyramids FC) na Issoufou Dayo (RS Berkane).
Sambamba na hilo klabu anayoichezea Kapombe ya Simba nayo imo katika tuzo hizo ikiwania katika kipengele cha klabu bora 2025 na klabu za Pyramids (Misri), RS Berkane (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Orlando Pirates (Afrika Kusini), Stellenbosch (Afrika Kusini) na Al Hilal (Sudan).
Kwa upande wa Mayele mbali ya kuwania tuzo ya mchezaji bora kwa Inter Club, jina lake pia limo kwa wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka akichuana na Mohamed Salah wa Liverpool na Achraf Hakimi wa PSG.

Wachezaji wengine waliomo kwenye kipengele hicho ni Andre Zambo-Anguissa (Napoli), Denis Bouanga (Los Angeles FC), Serhou Guirassy (Borussia Dortmund), Oussama Lamlioui (RS Berkane), Victor Osimhen (Galatasaray), Iliman Ndiaye (Everton) na Pape Matar Sarr (Tottenham Hotspur).
Katika kipengele cha kipa bora wa mwaka, hakuna kipa anayecheza soka Tanzania ambaye jina lake limo kwenye orodha hiyo ambapo waliomo ni Andre Onana (Trabzonspor), Vozinha (Chaves), Ahmed El Shenawy (Pyramids), Munir Mohamedi (RS Berkane), Yassine Bonou (Al Hilal), Stanley Nwabali (Chippa United), Edouard Mendy (Al Ahli), Ronwen Williams (Mamelodi Sundowns), Aymen Dahmen (CS Sfaxien) na Marc Diouf (Tengueth).
Kwa upande wa timu bora ya taifa, Morocco inawania tuzo hiyo ikiwakishwa na timu mbili ambazo ni timu ya wakubwa pamoja na ya vijana chini ya miaka 20.
Timu nyingine za taifa zinazowania tuzo hiyo ni Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Cape Verde, Ivory Coast, Afrika Kusini na Tunisia.
Katika makocha pia hakuna kocha anayefundisha Tanzania aliyemo katika orodha hiyo inayoongozwa na Hossam Hassan wa Misri, Bubista (Cape Verde), Pape Thiaw (Senegal), Krunoslav Jurcic (Pyramids), Sami Trabelsi (Tunisia), Romuald Rakotondrabe (Madagascar), Moine Chaabani (RS Berkane), Tarik Sektioui (Morocco), Mohamed Ouahbi (Morocco U-20) na Walid Regragui (Morocco).
