Stockholm, Sweden
Aliyekuwa kocha wa West Ham United, Graham Potter (50) ametangazwa kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya Sweden akiwa na jukumu la kuimarisha mbio za timu hiyo kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Sweden imekuwa ikisaka kocha mpya tangu wamtimue Jon Dahl Tomasson baada ya timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na Kosovo, mechi iliyochezwa Oktoba 13, matokeo yaliyoifanya timu hiyo iwe katika mazingira magumu ya kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia.
Mechi dhidi ya Kosovo ingawa matokeo yake yameiweka pagumu Sweden, timu hiyo bado inaweza kufuzu fainali hizo kupitia, play-offs hata kama haitomaliza katika nafasi mbili za juu za Kundi B na hiyo ni kutokana na mafanikio yao kwenye Nations Ligi walipomaliza kinara katika kundi lao
Kwa upande wake Potter amekubali jukumu la kuinoa timu hiyo kwa mkataba wa muda mfupi lengo likiwa ni moja tu, kuhakikisha anaibua matumaini na kuiwezesha Sweden kufuzu Kombe la Dunia.
Potter pia alisema kwamba ameipokea vizuri kazi ya kuinoa Sweden lakini pia amevutiwa na kazi hiyo akiamini kuwa Sweden ni timu yenye wachezaji wazuri ambao wanafanya vizuri katika ligi bora duniani kila wiki.
‘”Kazi yangu itakuwa ni kutengeneza mazingira ili timu iwe yenye kupata matokeo katika kiwango cha juu na kuipeleka Sweden kwenye Kombe la Dunia mwakani katika majira ya kiangazi,” alisema Potter.
Septemba mwaka huu Potter alitimuliwa West Ham baada ya kuwa na mwanzo mgumu katika msimu wa 2025-26 akiwa amepoteza mechi tano kati ya sita kabla ya hapo aliwahi kuzinoa timu za Brighton, Swansea City kabla ya kujiunga na Chelsea mwaka 2022 ingawa alitimuliwa baada ya kudumu kwa miezi saba.
