Na mwansishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeshindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kuchapwa bao 1-0 na Zambia katika mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Ikiwa kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar Jumatano, Oktoba 8, 2025, Stars ilikabiliana na Zambia au Chipolopolo kwa dakika 45 za kwanza na timu hizo kutoka uwanjani zikiwa hazijafungana.
Mambo yaliwaharibikia wenyeji Stars katika dakika ya 75, Zambia walipopata bao hilo pekee lililofungwa na Fashion Sakala kwa pasi ya Lubambo Musonda.
Kwa matokeo hayo, Stars inabaki na pointi zake 10 katika Kundi E ikiwa nafasi ya tatu, kundi ambalo Morocco inashika usukani ikiwa tayari imejikatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2026 ikiwa tayari imekusanya pointi 21.
Matokeo hayo pia ni dhahiri yatapokewa kwa mshangao na mashabiki wa Tanzania hasa baada ya timu yao kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia.
Stars pia inakuwa imefuta rasmi matumaini yake kwenye kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa kushindwa hata kufikia hatua ya play offs.
Nayo Zambia inakuwa imejiweka katika matumaini mapya kwa kufikisha pointi tisa na sasa inasubiri kucheza mchezo wa mwisho na Niger ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 12, pointi ambazo Zambia ikishinda itakuwa imezifikia na itashindana na Niger kwenye wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Timu nyingine katika kundi hilo ni Congo yenye pointi moja ambayo iliathiriwa na adhabu ya kufungiwa na Fifa na inayoshika mkia ni Eritrea ambayo haina pointi hata moja.
Kimataifa Zambia yaipiga Stars 1-0
Zambia yaipiga Stars 1-0
Read also
