Manchester, England
Bilionea na mmiliki mwenza wa klabu ya Manchester United, Sir Jim Ratcliffe amesema kocha wa timu hiyo, Ruben Amorim anahitaji miaka mitatu kuthibisha kwamba yeye ni kocha bora.
Kauli ya tajiri huyo imekuwa wakati huu ambapo mwezi ujao, Amorim atatimiza mwaka mmoja tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa Man United akitokea Sporting ya Ureno lakini timu imekuwa na matokeo yasiyovutia kiasi cha kuibua uvumi wa kufutwa kazi kwa kocha huyo.
Msimu uliopita Man United ilimaliza Ligi Kuu England (EPL) ikiwa nafasi ya 15, nafasi ambayo ni ya chini mno katika historia ya timu hiyo ikiwakumbusha hali iliyowakuta msimu wa 1973-74, timu hiyo ilipojikuta ikishuka daraja.
Hali imeendelea kuwa mbaya licha ya Pauni milioni 200 kutumika katika usajili na tayari wameshapoteza mechi tatu za EPL msimu huu lakini pia timu hiyo imetolewa kwenye michuano ya Kombe la EFL na timu ya Ligi Two ya Grimsby.
Kabla ya mechi ya wikiendi iliyopita dhidi ya Sunderland, mechi ambayo Man United ilishinda kwa mabao 2-0, habari kubwa ilikuwa ni kuhusu siku za kocha huyo kuhesabika na kwamba angetimuliwa wakati wowote.
Habari hizo zilikolezwa na Amorim mwenyewe ambaye alisema kibarua chake kipo hatarini kutokana na matokeo mabaya akisisitiza kuwa hawezi kamwe kuvumiliwa kama hatokuwa na matokeo mazuri.
Katika mahojiano ya hivi karibuni, Ratcliffe amekuja tofauti na mtazamo wa kumfuta kazi kocha huyo badala yake amesema suala la Amorim haliwasumbui na kufafanua kwamba kocha huyo anahitaji muda zaidi kudhihirisha ubora wake.
“Hana msimu mzuri, Ruben anahitaji kuthibitisha kuwa yeye ni kocha bora kwa kipindi cha miaka mitatu, hivyo ndivyo itakavyokuwa,” alisema Ratcliffe.
Amorim amekuwa akilaumiwa na wachambuzi mbalimbali kwa mfumo anaoutumia wa 4-3-2-1 kwa madai kwamba hauwezi kuipa ushindi timu hiyo lakini mwenyewe ameshikilia msimamo wake akikataa kubadili mfumo.
Kuhusu hoja hiyo, Ratcliffe alisema mazungumzo hayo hayamsumbui lolote akidai kwamba yanatokana na ujinga na zaidi ya hilo kuna wakati havielewi vyombo vya habari.
“Kuna wakati sivielewi vyombo vya habari, wanataka mafanikio ya ghafla, wanadhani ni kama kuwasha taa, wanajua ni kama kubonyeza swichi ya taa na kesho mambo yanakuwa mazuri, huwezi kuendesha klabu kama ya Manchester United kwa kauli za waandishi,” alisema Ratcliffe.
