Florida, Marekani
Kocha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni amesema hatokuwa tayari kumpa nafasi mchezaji wake Lionel Messi au mchazaji mwingine yeyote wa timu hiyo kama hatokuwa fiti asilimia 100 ili kumuepusha kumuweka katika hatari ya kuumia zaidi.
Timu ya taifa ya Argentina keshokutwa, Ijumaa Oktoba 10, 2025, itacheza mechi ya kirafiki na Venezuela, mechi ambayo itapigwa mjini Miami nchini Marekani kwenye Uwanja wa Hard Rock na Jumatatu inayofuata itaumana na Puerto Rico mjini Chicago.
Messi ambaye ni nahodha wa timu ya Argentina, kabla ya kujiunga na timu yake ya taifa, amekuwa na ratiba ngumu akiwa amecheza mechi saba katika siku 21 na timu yake ya Inter Miami ya Marekani.
Kwa kuliangalia hilo, Scaloni amesema kwamba watachukua uamuzi wa kuwa na mchezaji huyo au kumuacha yeye na wachezaji wengine baada ya kujua hali zao na kuwa na uhakika kama wapo fiti asilimia 100.
Uwezekano wa Massi na mchezaji mwenzake wa Inter Miami, Rodrigo De Paul kuwapo kwenye mechi na Venezuela upo katika hatihati kwa kuwa Inter Miami ina mechi muhimu ya ligi ya MLS dhidi ya Atlanta United siku moja baada ya mechi ya Argentina na Venezuela.
“Tutazungumza na Messi na wachezaji wengine, nia ni kuhakikisha hatuwaweki katika mazingira ya hatari, hizi ni mechi muhimu kwa timu ya taifa lakini ni za kirafiki, mchezaji yeyote mwenye majeraha madogo awe Messi au mwingine yeyote hatuwezi kumchukua na kumuweka katika hali ya hatari,” alisema Scaloni.
Katika msimu huu pekee, Messi tayari ameifungia Inter Miami mabao 24 na kutoa asisti 17 na jana Jumanne mchana alionekana akifanya mazoezi na timu ya taifa ya Argentina kwenye uwanja wa mazoezi wa Inter Miami.
Scaloni pia alisema mechi zijazo za Argentina anataka kuzitumia kwa kuwapa nafasi wachezaji wapya kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia mwakani.
