Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limewateua Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Walace Karia na Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said katika kamati za shirikisho hilo nafasi ambazo watazitumikia kwa miaka minne.
Katika uteuzi huo, Karia ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ameteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati ya Fifa ya soka la ufukweni, kamati inayojihusisha na maendeleo ya soka la ufukweni duniani.
Kwa upande wa Hersi ambaye pia ni Rais wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA) ameteuliwa kwenye kamati ya mashindano ya Fifa ambayo jukumu lake ni kusimamia na kuratibu maendeleo ya michuano ya kimataifa ya klabu duniani.
Sambamba na viongozi hao, Fifa pia wamemteua mwanamama Neema Haji ambaye ni meneja wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ kuwa mjumbe wa kamati ya Fifa ya mashindano ya soka la wanawake.
Uteuzi wa viongozi hao watatu kwenye kamati za Fifa unatoa picha ya namna ambavyo soka la Tanzania limeendelea kupiga hatua kuanzia ngazi ya klabu na timu ya taifa.
Uteuzi wa Karia kwa kiasi kikubwa umechangiwa na mafanikio ya timu ya taifa na klabu za Yanga na Simba kwenye mashindano ya klabu Afrika na maendeleo ya soka la ufukwenu nchini Tanzania.
Kuhusu Hersi klabu anayoiongoza ya Yanga imekuwa gumzo barani Afrika kutokana na mafanikio yake katika miaka ya hivi karibuni kwenye ligi kuu nchini na michuano ya klabu Afrika.
Kwa upande wa Neema, mchango wake katika soka la wanawake umejidhihirisha hasa kwenye Twiga Stars, timu ambayo katika miaka ya karibuni imekuwa yenye kutoa ushindani tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kimataifa Karia, Hersi waula Fifa
Karia, Hersi waula Fifa
Read also
