Na mwandishi wetu
Beki Ibrahim Abdullah ‘Ibra Bacca’ wa Yanga amefungiwa mechi tano za Ligi Kuu NBC kwa kosa la kumchezea rafu Ibrahim Ame wa Mbeya City katika mechi baina ya timu hizo iliyopigwa Jumanne Septemba 30, 2025 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Taarifa ya kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa maamuzi hayo baada ya kupitia mwenendo wa mechi za ligi katika kikao chake kilichofanyika Alhamisi, Oktoba 2, 2025.
Katika taarifa yake kamati hiyo imeitaja rafu ya Bacca kwa Ame kuwa ni ya makusudi, mbaya na ambayo ingeweza hata kuhatarisha usalama wa mchezaji huyo.
Naye mwamuzi wa mchezo huo, Omary Mdoe kutoka Tanga, ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano ya mechi za ligi hiyo kwa kosa la kushindwa kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua.
Mwamuzi huyo pia ametajwa kushindwa kuchukua hatua katika dakika ya 46 baada ya mchezaji wa Mbeya City, Matheo Anthony kuunawa mpira ndani ya eneo la penalti lakini hakuchukua hatua yoyote katika mechi hiyo iliyoisha kwa timu hizo kutoka sare.
Naye Mohamed Bakar wa JKT Tanzania amefungiwa mechi tano za ligi hiyo kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda katika mechi baina ya timu hizo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Sambamba na mchezaji huyo, waamuzi wa mchezo huo Jackson Samweli wa Arusha ambaye alikuwa mwamuzi wa kati na mwamuzi msaidizi namba 2, wote wamesimamishwa kwa mizunguko mitano kwa kosa la kushindwa kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua.
Nazo klabu za Pamba Jiji na Dodoma Jiji kila moja imetozwa faini ya Sh milioni tano, Dodoma Jiji kwa kosa la kuanza msimu wa ligi bila ya kuwa na kocha mwenye ujuzi na Pamba kwa kosa la kuweka picha ya video kwenye mitandao yao ya kijamii ikiwaonesha wachezaji wakifanya mazoezi gizani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Pamba waliokuwa wakijiandaa kucheza na Yanga, mechi ambayo walifungwa mabao 3-0, kitendo chao cha kuweka picha hiyo kimetajwa kuwa kilizua taharuki na kuchafua taswira ya ligi huku ikikosekana misingi hasa ya kufanya hivyo.
Katika adhabu nyingine timu ya KMC imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la ubao wao wa kuonesha matokeo kwenye uwanja wao wa nyumbani wa KMC Complex kutofanya kazi wakati wa mechi yao na Dodoma Jiji, mechi ambayo KMC walilala kwa bao 1-0.
Soka Ibra Bacca afungiwa mechi 5
Ibra Bacca afungiwa mechi 5
Related posts
Read also
