Liverpool, England
Beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher (pichani) hafurahishwi na staili ya uchezaji ya timu hiyo ambayo amesema inafanana na timu ya mpira wa kikapu (basketball) na kumtaka kocha Arne Slot aweke mambo sawa ili awe na haki ya kulipwa fedha zake.
Katika mechi yake ya mwisho Jumanne, Liverpool ililala kwa bao 1-0 mbele ya Galatasaray kwa bao pekee la Victor Osimhen kwa mkwaju wa penalti lakini hapo kabla timu hiyo ilishindwa kutamba mbele ya Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England (EPL).
Akifafanua kuhusu hoja yake hiyo, Carragher ambaye pia aliichezea timu ya taifa ya England alisema kwamba anachokiona kwa Liverpool ni timu inayocheza kama ya mpira wa kikapu kwa kucheza mwanzo hadi mwisho na hadhani kama timu kubwa inacheza hivyo.
“Na wakienda mbele hakuna wanachokipata lakini hapo hapo kwenye ulinzi wanapoteza sana, kwa sasa namfikiria kocha, msimu uliopita ulikuwa mteremko kwao na kwa sasa anatakiwa kupigania fedha zake,” alisema Carragher.
Katika mechi ya Jumanne dhidi ya Galatasaray iliyopigwa katika jiji la Istanbul, Liverpool walikuwa na wakati mgumu mbele ya mashabiki wa timu mwenyeji lakini kwa Carragher kipigo cha bao 1-0 walichokipata si jambo la kushtua kwani kilishaonekana na hivyo ni jukumu la kocha kuweka mambo sawa.
Carragher pia alimzungumzia mchezaji mpya wa timu hiyo, Florian Wirtz ambaye amesajiliwa bei mbaya akimtaka kuthibitisha thamani yake kwani hadi sasa hajaifungia timu hiyo bao lolote kwenye EPL na Ligi ya Mabingwa na katika mechi na Galatasaray alionekana kuwa na wakati mgumu.
Akifafanua zaidi Carragher alisema kwake Liverpool ni kama janga kwa kuwa si suala la kupoteza mechi au kufungwa kwani yote hayo alishayaona mapema na kusisitiza kuwa kocha anatakiwa kuijenga timu, kuwafanya wachezaji wajiamini, kuimarisha ulinzi na kuirudisha timu kama ya msimu uliopita.
