London, England
Kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa England kwa msimu uliopita wa 2024-25 akiwashinda Declan Rice aliyeshika nafasi ya pili na Harry Kane, nafasi ya tatu.
Bellingham, 22, alifunga mara moja katika mechi nane za England katika Nations League wakati timu hiyo ikiwa chini ya kocha wa muda, Lee Carsley kabla ya timu hiyo kuanza mbio za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 chini ya kocha mpya, Thomas Tuchel.
Kwa kutwaa tuzo hiyo, Bellingham, anakuwa mchezaji wa pili anayecheza soka nje ya England kubeba tuzo hiyo akitanguliwa na Owen Hargreaves ambaye alishinda mwaka 2006 wakati akiichezea Bayern Munich ya Ujerumani.
Katika Nations League, Oktoba 2024, Bellingham alifunga bao dhidi ya Ugiriki na akatoa asisti mbili na kusababisha penalti katika mechi na Jamhuri ya Ireland kabla ya kutoa asisti nyingine katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Albania.
Bellingham kwa sasa yuko fiti baada ya kuandamwa na matatizo ya bega takriban miezi mitatu iliyopita na Oktoba 9 anatarajia kuiwakilisha England katika mechi dhidi ya Wales na Oktoba 14 katika mechi na Latvia.
Na kwa mwaka jana tuzo hiyo ilichukuliwa na Cole Palmer wakati Bukayo Saka yeye alishinda tuzo hiyo mara mbili mfululizo kabla ya Palmer.
Mshindi wa tuzo hiyo kwa upande wa wanawake anatarajiwa kutajwa baadaye huku jina la Alessia Russo likiwamo katika orodha ya wachezaji 18 ambapo mchezaji huyo amekuwa akitajwa zaidi baada ya kuiwezesha timu ya wanawake ya England kubeba Kombe la Ulaya mara mbili mfululizo.
Kimataifa Bellingham mchezaji bora wa mwaka
Bellingham mchezaji bora wa mwaka
Read also
