Na mwandishi wetu
Timu za soka za Yanga na Singida Big Stars leo Jumamosi, Septemba 27, 2025 zimetamba katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na hivyo kusonga mbele hatua ya pili.
Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, iliilaza Wiliete FC ya Angola mabao 2-0 na hivyo kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya ushindi wa awali wa ugenini wa mabao 3-0.
Katika mechi hiyo Yanga leo ilianza mechi kwa tabu na hadi dakika 45 za awali zinamalizika hakuna timu iliyopata bao jambo lililoonekana kuwakera baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wakionekana kutozifurahia mbinu za kocha Folz.
Yanga iliandika bao la kwanza dakika ya 70 mfungaji akiwa Pacome Zouzoua akiitumia vizuri pasi ya Andy Boyell kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 86, bao lililofungwa kwa kichwa na Aziz Andabwile kwa kona iliyochongwa na Often Chikola.
Kwa ushindi huo, Yanga sasa itaumana na Silver Strikers ya Malawi, mechi ambayo inatarajiwa kuchezwa kati ya Oktoa 17 na 19 ambapo Yanga itaanzia ugenini na kurudiana wiki moja baadaye jijini Dar es Salaam.
Nao Singida BS wakiwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam walifanikiwa kuilaza APR ya Rwanda mabao 3-1 na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 baada ya ushindi wa mechi ya awali wa bao 1-0.
Kwa ushindi huo, Singida BS inayoshiriki Kombe la Shirikisho, katika mechi za hatua ya pili inasubiri kuumana na mshindi wa mechi kati ya Al Akhdar ya Libya na Flambeau ya Burundi, mechi itakayochezwa Jumapili.
Wakati huo huo mambo si mazuri kwa Mlandege ya Zanzibar licha ya ushindi wa mabao 3-2 iliyoupata leo dhidi ya Ethiopia Insurance ya Ethiopia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo imetolewa kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya kulala kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza.
Kimataifa Yanga, Singida BS zang’ara CAF
Yanga, Singida BS zang’ara CAF
Read also
