Na mwandishi wetu
Simba imeanza na ushindi mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu NBC kwa kuipa kichapo cha mabao 3-0 Fountain Gate FC mechi iliyopigwa Alhamisi hii Septemba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Washindi walianza kusaka bao la mapema na juhudi hizo kuzaa matunda dakika ya tano ya mchezo huo kwa bao lililofungwa na Rushine De Reuck akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Jean Ahoua.
Dakika 10 kabla ya timu kwenda mapumziko, Simba waliandika bao la pili mfungaji akiwa Ahoua ambaye alifunga bao hilo kwa pasi ya Yusuf Kagoma na kuzifanya timu ziende mapumziko Simba wakiwa mbele kwa mabao mawili.
Ahous mmoja wa wachezaji walioonesha ubora katika kikosi cha Simba msimu uliopita, pia ndiye aliyetangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kipindi cha pili mambo yalizidi kuwa magumu kwa Fountain Gate ambao walipachikwa bao la tatu mfungaji akiwa Jonathan Sowah aliyefunga bao hilo dakika ya 57 kwa pasi ya Elly Mpanzu.
Simba ingeweza kupata mabao mengi katika mechi hiyo kama si ubutu wa safu ya ushambuliaji kwani licha ya kutengeneza nafasi kadhaa lakini umaliziaji ilikuwa tatizo.
Baada ya ushindi huo, Simba sasa inasubiri kucheza mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, mechi itakayocheza Jumapili ijayo, Septemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya kwanza, Simba ikiwa ugenini ilitoka na ushindi wa bao 1-0, mechi ambayo ilikuwa ya mwisho kwa aliyekuwa kocha wao, Fadlu Davids ambaye ameachana na Simba na kujiunga na Raja Casablanca ya Morocco.
Soka Simba yaicharaza Fountain Gate 3-0
Simba yaicharaza Fountain Gate 3-0
Read also
