Na mwandishi wetu
Yanga ya Tanzania imeanza vyema mbio za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuichapa Wiliete FC ya Angola mabao 3-0 mechi iliyochezwa leo, Ijumaa, Septemba 19, 2025 kwenye Uwanja wa 11 Novembro mjini Luanda, Angola.
Yanga walianza kuzitikisa nyavu za wenyeji wao Wiliete dakika ya 32 kwa bao la Aziz Andambwile aliyefunga kwa shuti la nje ya 18 kwa mpira uliokwenda moja kwa moja wavuni na kumshinda kipa, Agustino Kalougha licha ya kujaribu kuurukia.
Bao hilo halikuonekana kuwashtua Wiliete na kufanya juhudi za kusaka bao licha ya kuwa kwenye uwanja wa nyumbani, badala yake timu hiyo iliendelea kuchezewa nusu uwanja huku wachezaji wake wakiwa na kazi ya ziada ya kuokoa mashambulizi ya Yanga.
Kipindi cha pili Yanga waliendelea kufanya mashambulizi kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza lakini ubutu wa safu ya ushambuliaji uliendelea kujidhihirisha hadi walipojirekebisha na kupata bao la pili dakika ya 72 mfungaji akiwa Edmund John kwa pasi ya Maxi Nzengeli.
Dakika 10 baadaye Yanga walikamilisha hesabu yao ya mabao na kufikia matatu baada ya Prince Dube kuzichana nyavu akiwa ndani ya eneo la 18 na hivyo kuzidi kufifisha matumaini ya Wiliete, timu iliyoanzishwa miaka sita iliyopita.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo ingawa inasubiri kurudiana na timu hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ijayo.
Kimataifa Yanga yatakata Angola
Yanga yatakata Angola
Read also
