Manchester, England
Mshambuliaji kinara wa mabao Man City, Erling Haaland amevunja rekodi nyingine Alhamisi hii Septemba 17, 2025 kwa kufunga mabao 50 katika mechi chache za Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko mchezaji yoyote katika historia ya mashindano hayo.
Haaland aliiongoza vyema Man City katika mechi dhidi ya Napoli na kufunga bao katika Uwanja wa Etihad na hivyo kufikisha mabao 50 katika mechi 49 za michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Ulaya na duniani.
Wachezaji wengine waliofikisha mabao 50 katika michuano hiyo ni nyota wa zamani wa timu za Man United na Real Madrid, Cristiano Ronaldo na Ruud van Nistelrooy ambao walifikisha idadi hiyo ya mabao katika mechi 62,
Naye Lionel Messi alifikisha idadi kama hiyo katika mechi 66 ingawa anabaki na rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha idadi kama hiyo ya mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, aliifikisha akiwa na miaka 24.
Kwa rekodi hiyo, Haaland pia anakuwa amewapiku kwa mabao magwiji wa zamani Ulaya kwenye ligi ya mabingwa na Kombe la Ulaya ambao ni Alfredo di Stefano wa Real Madrid na Zlatan Ibrahimovic ambaye amechezea timu tofauti tofauti.
Haaland kwa mabao hayo pia anakuwa sawa na Filipo Inzaghi na amezidiwa bao moja na Thierry Henry huku Ronaldo akiendelea kuwa namba moja kwa mabao mengi katika ligi hiyo, mabao 141, nafasi ya pili ikishikiliwa na Messi mwenye mabao 129.
“Nini ninachoweza kusema? Namba zinazungumza zenyewe, tuna bahati ya kuwa naye, wapo kina Van Nisterlrooy, Lewandowski pamoja na Cristiano na Messi watu wawili hatari, Erling kuwa katika kundi hilo ni jambo ambalo huwezi kuamini,” alisema kocha wa Man City, Pep Guardiola.
