Paris, Ufaransa
Nyota wa zamani wa Man United na timu ya taifa ya Ufaransa, Eric Cantona ameyataka mashirikisho ya soka duniani (Fifa) na Ulaya (Uefa) kuzipiga marufuku timu za Israel kushiriki mashindano yanayoandaliwa na mashirikisho hayo.
Cantona (pichani juu) ametoa msimamo huo kwa sababu ya matukio ya mauaji yanayoendelea Gaza yakifanywa na Israel dhidi ya raia wa Palestina na kusisitiza kuwa Fifa na Uefa wanatakiwa kuwa na msimamo dhidi ya Israel.
Shirika la haki za binadamu duniani la Amnesty International pamoja na Umoja wa Mataifa kwa pamoja uchunguzi wao umebaini kuwa Israel inafanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika ukanda wa Gaza.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameonekana kutotikisika kwa namna yoyote na kinachoendelea Gaza licha ya kushutumiwa kila kona duniani kote.
Netanyahu badala yake ameendelea kutoa maagizo ya kuendeleza mashambulizi Gaza huku ukiukwaji wa haki za kibinadamu ukiendelea siku hadi siku na hivyo kusababisha kuwapo hoja za kutaka Israel iwekewe vikwazo.
Kuwapo kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadam hakujaishtua Fifa kwani timu ya taifa ya Israel kwa sasa inapambana katika kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, mashindano ambayo mara ya mwisho taifa hilo lilishiriki mwaka 1970.
Sambamba na hilo klabu ya Maccabi Haifa ya Israel nayo inashiriki michuano ya Europa Ligi ambayo inasimamiwa na Uefa.
Cantona amekuwa mstari wa mbele katika harakati za kisiasa na Jumatano hii usiku wa Septemba 17, 2025 alishiriki kwenye tamasha maalum lililopewa jina la Pamoja kwa Ajili ya Palestina, tamasha lililofanyika jijini London.
Katika tamasha hilo, Cantona alizungumza bila hogu akiwataka Fifa na Uefa kuchukua hatua dhidi ya Israel kama ambavyo wamewahi kuichukulia hatua Urusi kwa kitendo chake cha kuivamia Ukraine.
“Nimeichezea Ufaransa na Manchester United, najua soka la kimataifa ni zaidi ya michezo, ni utamaduni, ni siasa na pia kuna nguvu za aina fulani,” alisema Cantona.
Cantona alisema kwa namna ambavyo nchi inajiwakilisha kimataifa wakati umefika wa kuifungia Israel katika hadhi hiyo ya kimichezo kimataifa kama ilivyokuwa kwa Urusi ambayo siku nne tu baada ya kuivamia Ukraine, Fifa na Uefa waliifungia nchi hiyo.
Nyota huyo aliyetamba zaidi katika soka miaka ya 1990 mwanzoni, alisema tayari siku 716 zimepita katika kile ambacho Amnesty International wamekitaja kuwa ni mauaji ya halaiki lakini Israel wanaendelea kuruhusiwa kushiriki katika michezo.
