Na mwandishi wetu
Singida Black Stars ya Tanzania imeuanza kwa kishindo msimu wa 2025-26 kwa kubeba taji la michuano ya klabu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) maarufu Kombe la Kagame kwa kuinyuka Al Hilal ya Sudan mabao 2-1.
Shujaa wa Singida BS katika mechi hiyo ya fainali iliyipigwa Jumatatu hii Septemba 15, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam alikuwa ni kiungo mpya wa timu hiyo, Clatous Chama aliyefunga mabao yote mawili.
Chama aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Yanga, alifunga mabao hayo kipindi cha kwanza na cha pili, alianza kuandika bao la kwanza dakika ya 21 lakini Al Hilal walipambana na kusawazisha bao hilo dakika ya 31 kupitia kwa Abdelrazaq Taha.
Kipindi cha pili timu zote zilikianza kwa kasi zikisaka bao la ushindi lakini alikuwa ni Chama aliyewainua vitini mashabiki wa Singida alipoandika bao la pili na la ushindi kwa shuti lililomshinda kipa Soufiane Farid wa Al Hilal.
Ushindi wa Singida unakuwa mwanzo mzuri kwa Chama na nyota mwenzake waliyekuwa naye kutokea Yanga, Khalid Aucho ambao wameungana kwa mara nyingine na kocha wao wa zamani wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye kwa sasa anainoa timu hiyo.
Akizungumzia ushindi huo, Gamondi alisema kwamba timu yake ilicheza kwa nidhamu na ana furaha kwa kuibuka washindi akiwa na timu hiyo mpya ambayo ndiyo mara ya kwanza inabeba taji lenye hadhi ya kimataifa.
Kwa ushindi huo, Singida BS wameondoka na kitita cha Dola 30,000 pamoja na medali ya dhahabu wakati Al Hilal walioshika nafasi ya pili wamepata Dola 20,000 na medali ya fedha.
APR ya Rwanda imeshika nafasi ya tatu baada ya kuinyuka KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam bao 1-0 na kukabidhiwa medali ya shaba pamoja na Dola 10,000.
Kwa upande mwingine nyota wa APR, Raouf Dao Memel ametangazwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo wakati tuzo ya mfundaji bora ikienda kwa Chama wa Singida na kipa bora ni Metacha Mnata wa Singida huku Al Hilal wakibeba tuzo ya Fair Play.
Michuano hiyo ilishirikisha timu kutoka Tanzania Bara, Kenya, Somalia, Zanzibar, Djibouti, Brurundi, Ethiopia, Rwanda, Sudan Kusini na Sudan.
Kimataifa Singida Black yabeba taji Cecafa
Singida Black yabeba taji Cecafa
Read also
