Na mwandishi wetu
Bao pekee la Pacome Zouzoua limeifanya Yanga kuendelea kuwanyanyasa mahasimu wao Simba kwa kutoka na ushindi wa 1-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa leo Jumanne Septemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
Huu ni ushindi wa sita mfululizo wanaupata Yanga dhidi ya Simba lakini ushindi wa leo umekuwa mtamu baada ya Yanga kubeba Ngao ya Jamii na hivyo kuashiria mwanzo mzuri wa timu hiyo katika msimu mpya wa 2025-26 ambao pazia lake limefunguliwa rasmi kwa mechi hiyo.
Yanga inabeba taji hilo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo wakati wakiukaribisha msimu uliopita wa 2024-25 kwa kuichapa Azam FC mabao 4-1.
Ushindi wa leo ulipatikana katika dakika ya 53 baada ya kipa wa Simba, Muosa Camara kushindwa kuumiliki mpira uliopigwa na Maxi Nzengeli na kumkuta Pacome ambaye alionesha utulivu na kupiga mpira uliojaa wavuni.
Timu zote ziliuanza mchezo kwa kasi na kuonesha shauku ya kutaka ushindi huku Kibu Denis akishindwa kuipatia Simba bao dakika ya 27 na beki Shomari Kapombe akishindwa kuitumia vyema nafasi aliyoipata dakika ya 40, Kibu na Kapombe wakiwa karibu na kipa Djigui Diarra walipiga mashuti yaliyotoka nje ya lango.
Yanga nao walifanya shambulizi la maana kipindi hicho hicho lakini mshambuliaji wake Prince Dube alishindwa kuunganisha vizuri krosi iliyochongwa na Aziz Andambwile kwa kuupiga mpira kwa bega na hivyo kudakwa kiulaini na kipa wa Simba, Camara.

Dakika chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza, kipa wa Yanga, Djigui Diarra alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Seleman Mwalimu na hivyo kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa hazijafungana.
Kipindi cha pili Yanga walikianza kwa kufanya mabadiliko kwa kumtoa Mudathir Yahya na nafasi yake kuingia Mamadou Doumbia mabadiliko ambayo yalionekana kuongeza kasi ya mchezo kabla ya Yanga kupata bao la Pacome.
Bao hilo lilionekana kuitia hasira Simba ambayo iliongeza kasi ya mashambulizi lakini ukuta wa Yanga chini ya Ibrahim Bacca na wenzake ulikuwa imara katika kuhakikisha mashambulizi hayo hayaleti madhara.
Yanga iliendelea kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili kwa kuwatoa, Shadrack Boka, Maxi Nzengeli, Duke Abuya na Prince Dube na kuwaingiza, Balla Conte, Celestine Ecua, Clement Mzize na Mohamed Hussein.
Simba nao katika mabadiliko yao waliwatoa Elly Mpanzu, Stephen Mukwala na Allasane Cante na nafasi zao kuchukuliwa na Neo Maena, Anthony Mligo na Mwalimu.
