Na mwandishi wetu
Yanga imefanya tamasha la kila mwaka la Siku ya Mwananchi kwa kuichapa Bandari ya Kenya bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. ushindi ambao ulitanguliwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali nchini.
Kilele cha Siku ya Mwanchi, ni tukio linaloashiria kuufungua msimu mpya kwa kutangaza kikosi kipya cha timu hiyo mbele ya mashabiki na kwa mwaka huu wa 2025, lilifanyika Ijumaa hii, Septemba 12, 2025.
Yanga walipata bao hilo pekee mapema dakika ya pili ya mchezo huo mfungaji akiwa ni nyota mpya wa timu hiyo, Celestine Ecua ambaye aliunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Prince Dube na kumshinda kipa wa Bandari, Allain Ngeleka.
Kasi ya Yanga kusaka bao la pili ilionekana dakika chache kabla ya mapumziko baada ya beki wao wa kushoto, Shadrack Boka kuambaa na mpira kwa kasi na kupiga shuti ambalo lilizuiwa na Sharif Majabe.
Matarajio ya mashabiki wa Yanga waliofurika uwanjani kuona timu yao ikiongeza mabao hayakuweza kufikiwa kwani hadi mwamuzi anamaliza mchezo dakika ya 90, Yanga walitoka uwanjani na bao hilo pekee la ushindi.
Kabla ya mechi hiyo, Siku ya Mwananchi ilipambwa na matukio kadhaa ya kijamii yaliyofanyika awali yakihusisha viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.
Baada ya matukio hayo, siku yenyewe ya Mwananchi kwenye Uwanja wa Mkapa, mashabiki wa Yanga walifurika kwenye Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya kuiona timu yao mpya ya msimu wa 2025-26 ambayo ndiyo iliyocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na Bandari.
Katika utambulisho huo, Yanga pia walitumia nafasi hiyo kutambulisha kwa mashabiki wao kikosi cha timu ya wanawake kabla ya ile ya wanaume sambamba na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwamo Zuchu na Dogo Patern.
Kimataifa Yanga yainyuka Bandari Kenya 1-0
Yanga yainyuka Bandari Kenya 1-0
Read also
