Manchester, England
Klabu ya Man United imethibitisha kuwa kipa wao, Andre Onana (pichani) amejiunga na klabu ya Trabzonspor ya nchini Uturuki kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Uamuzi wa Onana kujiunga na klabu hiyo inayocheza Ligi Kuu Uturuki au Super League, umekuja baada ya kuwa katika kikosi cha Man United kwa kipindi cha miaka miwili ambacho kimekuwa na hali ya kupanda na kushuka kwa umahiri wake.
Habari za ndani zinadai kuwa katika mkataba wa Onana kucheza Trabzonspor ada yake haikuwekwa wazi na hakuna kipengele kinachompa nafasi ya kusajiliwa moja kwa moja hivyo baada ya mwaka mmoja atarudi Man United.
Zaidi ya hilo, katika mkataba huo kwa kipindi chote atakachokuwa Trabzonspor, Man United haitowajibika kumlipa chochote kipa huyo ambaye pia huidakia timu ya taifa ya Cameroon.
Uamuzi wa Onana kukubali kuondoka Man United unaaminika kuwa umetokana na kitendo cha klabu hiyo kumsajili kipa Senne Lammens kutoka Antwerp katika siku za mwisho za usajili licha ya Onana kuahidi kubaki kwa lengo la kupigania nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Onana, 29, alijiunga na Man United mwaka 2023 akitokea Inter Milan ya Italia kwa ada iliyofikia Dola 59 milioni huku akipewa matumaini makubwa ya kuwa kipa tegemeo lakini kwa kipindi chote mwenendo wake umekuwa wa kupanda na kushuka ubora.
Taarifa fupi ya Man United ilieleza, “Kipa wa Manchester United, Andre Onana amejiunga na klabu ya Trabzonspor kwa mkopo katika kipindi chote cha msimu wa 2025-26.”
Onana ambaye amejiunga na Trabzonspor wakati wa siku za mwisho za dirisha la usajili Uturuki yaani Ijumaa hii Seotemba 12, 2025, akiwa Man United ameichezea timu hiyo mara 102 na kuiwezesha kubeba Kombe la FA mwaka 2024 wakati huo kocha akiwa Erik ten Hag.
Kimataifa Onana atimkia Uturuki
Onana atimkia Uturuki
Read also
