London, England
Joao Mendes (pichani) ambaye ni mtoto wa mwanasoka wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Ronaldinho au Gaucho, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea klabu ya Hull City inayoshiriki Ligi ya Champioship ua England.
Hull City wamearifu kuwa Mendes ambaye ana umri wa miaka 20 sasa, amejiunga na timu hiyo katika kikosi cha vijana chini ya miaka 21, akiwa mchezaji hutu baada ya kumaliza mkataba na klabu ya Burnley pia ya England.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Mendes alisema kwamba ana furaha kuwa katika timu hiyo kwa ajili ya kucheza soka huku akiwa na matumaini ya msimu kuwa mzuri kwake.
Mendes alisema kwamba ana uhakika Hull City ni timu nzuri kwake na anaamini atayafurahia mambo yajayo akiwa mmoja wa wachezaji katika timu hiyo.
Akiwa na Burnley msimu uliopita, Mendes ambaye ni winga anayecheza zaidi ya nafasi moja, aliichezea timu hiyo mechi tano kwenye kikosi cha vijana chini ya miaka 21.
Mendes ni jina lililoibukia kwao Brazil katika timu ya vijana ya Cruizero aliyoichezea hadi Machi 2023 kabla ya kufuata nyayo za baba yake kwa kujiunga na timu ya vijana ya Barcelona ambayo pia aliachana naye na kuhamia Burnley na sasa Hull City.
“Nafikiri ni vizuri kucheza soka kwa staili tofauti, Brazil wana staili yake, Hispania ni nyingine na England pia ni nyingine, kwa hiyo nafikiri ni faida katika soka kwa mtu anayecheza sehemu tofauti,” alisema Mendes.
Baba yake Mendes aliyefahamika zaidi kwa jina la Gaucho, enzi zake alishinda Kombe la Dunia mwaka 2002 na timu ya Brazil, akiwa Barcelona alishinda mataji ya La Liga mara mbili, taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja na mwaka 2005 alishinda tuzo ya Ballon d’Or.
