Na mwandishi wetu
Simba imeilaza Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 katika mechi maalum ya Tamasha ya Simba Day lililofanyika Jumatano hii, Septemba 10, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku msanii wa bongo fleva, Mbosso akinogesha tamasha hilo.
Kabla ya mechi hiyo kulikuwa na budurani mbalimbali zilizoteka maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo waliofurika uwanjani hapo kuanzia saa sita mchana wakifurahia utambulisho wa wachezaji na matukio mengine ya kuvutia.
Mashabiki hao kwa kiasi kikubwa waliupendezesha uwanja huo kwa jezi zao nyekundu, wengi wao wakiwa na jezi mpya za kampuni ya Jayrutty ambayo imeingia mkataba wa udhamini na Simba wenye thamani ya Sh bilioni 38.5.
Kwa kawaida tamasha la Simba Day ambalo lina miaka zaidi ya 10 sasa, hufanyika katika siku za mapumziko ya wiki yaani Jumamosi au Jumapili lakini mwaka huu limefanyika katikati ya wiki kutokana na muingiliano ya matukio ya kimichezo nchini Tanzania.
Ilitarajiwa mashabiki wangekuwa wachache lakini hali imekuwa tofauti, mashabiki wa Simba wameujaza Uwanja wa Mkapa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya 60,000 huku wakiupendezesha kwa jezi za rangi nyekundu.
Mbali na burudani ya muziki kutoka kwa Mboso ambaye aliimba nyimbo zake nyingi zinazopendwa pia ilikuwapo bendi maarufu ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta pamoja na DJ maarufu DJ Sinyorita, mwanadada ambaye naye alipokewa vyema na mashabiki wa klabu hiyo.
Burudani nyingine iliyokuwa kivutio kwa mashabiki wa Simba ni mechi ya wachezaji wa zamani wa timu hiyo yaani Veterans waliocheza na KT Veterans, mechi ambayo iliisha kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.
Katika mechi hii, mashabiki wa Simba walipata fursa ya kuwaona kwa mara nyingine nyota wao wa zamani wakionesha ubora wao wakiwamo Mussa Hassan Mgosi, Juma Jabu, Emmanuel Gabriel, Haruna Moshi ‘Boban’, Said Sued, Duwa Said na wengineo.
Matukio hayo na mengineyo kwa pamoja yamelifanya tamasha la Simba Day kuwa moja ya matukio makubwa ya kimichezo na burudani nchini kwa namna ambavyo limewakutanisha wana Simba wenye hadhi tofauti.
Katika tamasha hilo, ukiacha mashabiki waliofika uwanjani, wapo mashabiki wengine wengi kote Tanzania ambao walikuwa wakifuatilia tukio hilo moja kwa moja kwenye televisheni wakiwa majumbani mwao au kwenye kumbi za starehe.
Katika mechi na Gor Mahia, mabao ya Simba yalifungwa na Abdulrazak Hamza katika dakika ya sita wakati bao la pili lilifungwa na Steven Mukwala dakika ya 65.
Soka Mbosso anogesha Simba Day, Gor yapigwa 2-0
Mbosso anogesha Simba Day, Gor yapigwa 2-0
Read also
